Haya yameelezwa kwenye mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo ya ECOWAS ulioanza jana Jumapili mjini Abuja, Nigeria.
Rais wa Halmashauri kuu ya ECOWAS Oumar Touray amesema wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa Abuja kwamba ukanda huo unakabiliwa na kitisho cha kugawanyika na kuongezeka kwa mashaka ya kukosekana kwa usalama baada ya mataifa hayo matatu kusaini ushirika unaojulikana kama Alliance of Sahel States, AES.
Soma Pia: Mkutano wa ECOWAS wafanyika Abuja kutatua changamoto za kikanda
“Rais wa Halmashauri kuu ya ECOWAS Omar Touray: Hatushirikiani kwenye mipaka tu. Familia zetu zinajuana, jamii zetu zinashirikiana. Viongozi wanalenga kufanya kila liwezekanalo kuifanya jamii yetu kusimama pamoja. ECOWAS sio tu viongozi wa mataifa, ECOWAS ni jamii ya watu, ni jamii ya watu wanaotakiwa kuishi pamoja.”
Mkataba huo wa AES ulidhihirisha nia ya serikali hizo za kijeshi kujitoa kwenye muungano huo ulioanzishwa karibu miaka 50 iliyopita, baada ya kuvunja mahusiano ya kidiplomasia na kijeshi na mataifa ya magharibi, na sasa yakiimarisha ushirikiano na Urusi.
Soma pia: Wajumbe wa ECOWAS waelekea Togo wakati mivutano ikiongezeka
Burkina Faso, Niger na Mali zilichukua madaraka wakati kukishuhudiwa msururu wa mapinduzi ya kijeshi kati ya mwaka 2020 na 2023.
Bado haijulikani ni kwa umbali gani AES itasimamia sera ya kisiasa, kiuchumi na ulinzi katikati ya mapambano dhidi ya uasi wa Kiislamu uliodumu kwa muongo mmoja, na kwa upande mwingine kukuza uchumi kwenye mataifa hayo masikini zaidi ulimwenguni.
Kujiengua kwa mataifa hayo kunaweza kuidhoofisha jumuiya hiyo na kulingana na Touray, na kitisho kuanzia kwenye uhuru wa kutembea hadi soko la pamoja lililokutanisha karibu watu milioni 400 chini ya ushirika wa ECOWAS
Soma pia: Niger, Mali, Burkina Faso zaunda kikosi cha pamoja kupambana na uasi
ECOWAS yaiomba Senegal kuwa msuluhishi maalum
Jumuiya hiyo ilimchagua kwa mara nyingine Rais wa Nigeria Bola Tinubu, kuwa mwenyekiti wake kwa mwaka mmoja na kuwapa jukumu viongozi wa Senegal na Togo kusimamia juhudi za upatanishi na serikali hizo za kijeshi ili kujaribu kuwarejesha kwenye ushirika wa ECOWAS.
Viongozi hao wa ECOWAS walipitisha uamuzi wa kuhamasisha upatikanaji wa wanajeshi 5,000 wa kikanda watakaokuwa tayari kukabiliana na ugaidi. Kikosi hicho kilitarajiwa kuanza na brigedi ya wanajeshi 1,650, ambao wangeendelea kuongezwa kila wakati. Nchi wanachama zinatarajiwa kukifadhili kikosi hicho, lakini pia itauomba Umoja wa Afrika kuwasaidia kifedha.
Lakini kujiengua kwa mataifa hayo ni wazi kutazorotesha juhudi hizi.
Haijulikani bado hatua zinazoweza kuchukuliwa na jumuiya hiyo baada ya mkutano huu wa kilele wa Abuja, ingawa Rais wa Nigeria Bola Tinubu alimtolea wito kiongozi mpya wa Senegal kuwa kama “mjumbe maalumu” katika suala hili la upatanishi, bila ya kutoa maelezo zaidi.