Mahakama Kenya yaitoza Serikali faini mauaji ya raia wa Pakistan

Kajiado. Mahakama ya Kenya imebaini polisi wametenda kinyume cha sheria katika mauaji ya mwandishi wa habari wa Pakistan mwaka 2022 kutokana na malalamiko ya mjane wake, wakili wake na vyombo vya habari vya nchini Kenya.

Raia huyo wa Pakistan, Arshad Sharif, mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Pakistan na mfuasi wa Waziri Mkuu wa zamani, Imran Khan alipigwa risasi ya kichwa wakati Polisi wa Kenya walipolifyatulia risasi gari lake, Oktoba 2022.

Mjane wa mwandishi huyo, Javeria Siddique na makundi mawili ya wanahabari nchini Kenya waliwasilisha malalamishi mwaka 2023 dhidi ya viongozi waandamizi wa polisi na maofisa sheria kuhusu “mauaji ya kukusudia na kinyume cha sheria” ya Sharif na wahusika“ kutofanya uchunguzi”.

Leo Jumatatu, Julai 8, 2024, Mahakama Kuu ya Kajiado, mji ulio kusini mwa Nairobi, imekataa madai ya polisi kwamba mauaji hayo yalikuwa kesi ya utambuzi wa kimakosa na kwamba maofisa waliamini walikuwa wakilifyatulia risasi gari lililoibwa lililohusika kwenye utekaji nyara.

Jaji Stella Mutuku ametoa uamuzi kwamba mauaji ya Sharif yalikuwa kinyume na Katiba na kwamba haki zake za kuishi na kulindwa zilikiukwa, vyombo vya habari vya Kenya vimeripoti.

“Nimegundua kuwa watuhumiwa kwa pamoja kupitia vitendo vyao walikiuka haki za walalamikaji,” amesema Mutuku, kwa mujibu wa The Nation.

Wakili wa Siddique, Ochiel Dudley amethibitisha uamuzi wa Mahakama kwa AFP, akiuelezea kama “kielelezo cha uwajibikaji wa polisi”.

Amesema uamuzi huo umebaini “Kenya ilikiuka haki ya Arshad Sharif ya kuishi, utu na uhuru dhidi ya uteswaji, ukatili na kudhalilishwa”.

Amesema Mahakama imeamuru Serikali kulipa fidia ya Ksh10 milioni (Dola za Marekani 78,000).

Mahakama ya Kenya imesema Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma na Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi ilikiuka haki za Sharif kwa kutowashtaki maofisa wawili waliohusika, Dudley ameongeza.

Imeamuru taasisi hizo mbili kukamilisha uchunguzi wao na kuwafungulia mashtaka maofisa hao wawili wa polisi, amesema.

Sharif aliikimbia Pakistan Agosti 2022, siku chache baada ya kumhoji mwanasiasa mkuu wa upinzani ambaye alisema maofisa wa ngazi ya chini katika jeshi la Pakistan wanakiuka amri ambazo zilikwenda kinyume na “mapenzi ya wengi”.

Nchi hiyo imetawaliwa kijeshi kwa miongo kadhaa ya historia yake ya miaka 75 na ukosoaji wa taasisi ya usalama umeonekana kwa muda mrefu kama mstari mwekundu.

Related Posts