Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeshindwa kuendelea na ushahidi katika kesi ya kusafirisha vipande 413 vya meno ya tembo na kiboko, inayomkabili Hassan Likwena na wenzake watano kutokana na shahidi wa Serikali kupata udhuru na kushindwa kufika mahakamani.
Likwena na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu kwa kuuza, kukusanya, kununua kutakatisha fedha na kusafirisha nyara za Serikali ambazo ni meno 413 ya tembo na meno mawili ya viboko yenye thamani ya jumla ya Sh4.4bilioni, mali ya Serikali.
Wakili wa Serikali, Frank Rimoy ameieleza Mahakama hiyo leo Jumatatu, Julai 8, 2024 wakati kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 70/2022 ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.
“Mheshiwa hakimu, upande Jamhuri ulitarajia kuwa na shahidi mmoja, lakini kwa bahati mbaya shahidi huyo kutoka Handeni mkoani Tanga, amepata udhuru na kushindwa kufika mahakamani mwa sababu za kifamilia,” amedai Rimoy mbele ye Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamula na kuongeza;
“Kutokana na sababu hiyo, tunaiomba Mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa upande wa mashtaka.”
Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Hakimu Lyamula ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 17, 2024 na washtakiwa wamerudishwa rumande.
Mbali na Likwena, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Oliver Mchuwa, Haidary Sharifu, Joyce Thomas, Abdul Abdallah na Salama Mshamu ambao wanadaiwa kati ya Agosti 28, 2019 na Agosti 30, 2019 jijini Dar es Salaam, walijihusisha na genge la uhalifu kwa kuuza, kukusanya, kununua na kusafirisha meno 413 ya tembo na meno mawili ya viboko yote vikiwa na thamani ya Sh4.4bilioni, mali ya Serikali.
Pia, mshtakiwa Likwena na Abdallah, wanakabiliwa na shtaka matatu ya kutakatisha fedha, ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.