Safari ya milima, mabonde Padri Louis akitimiza miaka 105

Moshi. Wakati Padri Luois Shayo wa Jimbo Katoliki la Moshi, mwafrika wa kwanza kuwa Paroko wa jimbo akitimiza miaka 105 ya kuzaliwa, amesema kuishi kwake ni siri ambayo Mungu ameificha katika maisha yake.

Anasema amevuka milima na mabonde katika safari yake ya utume, lakini bado ana afya njema, jambo analomshukuru Mungu.

Padri huyo ambaye pia ni mwafrika wa 16  kupata upadri mwaka 1950, Juni 30, 2024 ametimiza miaka hiyo 105 na mwaka huu pia ametimiza miaka 74 ya upadri wake na huenda akavunja rekodi ya kuwa padri aliyeishi miaka mingi zaidi Barani Afrika.

Padri Louis ni miongoni mwa watoto tisa kwenye familia ya mzee Shayo wa Kijiji cha Imii, kilichopo Kilema wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro na kwa sasa anaishi katika nyumba ya mapadri wazee Longuo.

Akizungumza na Mwananchi Digital wakati Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alipokwenda kumtembelea kwenye makazi yake yaliyopo Longuo, padri huyo amesema hana cha kujivunia katika miaka yake hiyo 105, zaidi ya uhai ambao Mwenyenzi Mungu amemjalia kuishi hapa duniani.

Alipoulizwa nini siri ya yeye kuishi maisha marefu, padri huyo amesema Mungu amemjalia bahati na kwamba amemficha siri nyingi za maisha yake kuwa hivyo alivyo.

“Kufikisha miaka 105 ni Mungu tu, sina cha kujivunia zaidi ya uhai. Mungu amenijalia bahati ya kuishi hapa duniani, amenificha siri nyingi ya maisha yangu na ameniepusha na mabalaa mengi ambayo nimeyakwepa kwenye afya na utumishi wangu,” amesema Padri Louis.

Waziri Mkenda ambaye baada ya kufika nyumbani kwa padri huyo na kuzungumza naye faragha, amesema amefarijika kukutana naye kwa kuwa ni muda mrefu alitamani kumuona na kushiriki katika sherehe ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake.

“Nilipata taarifa kwamba Padri Louis alitamani kuniona na leo nimekuja kumuona, nimefarijika sana,” amesema Profesa Mkenda.

Amesema kuendelea kuishi kwa padri huyo ni baraka kwa Jimbo Katoliki la Moshi na hazina kwa kuwa mapadri wanajifunza mambo mengi kutoka kwake.

Akimzungumzia padri huyo, Wakili wa Askofu wa jimbo hilo, Padri Deogratius Matiika amesema Padri Luois ana historia katika maisha yake kwa kuwa ndiye aliyembatiza wakati akihudumia Parokia ya Mkuu iliyopo wilayani Rombo.

“Padri Luois pamoja na kugusa maisha ya wengi, binafsi amegusa maisha yangu kwa kuwa ndiye padri aliyenibatiza utotoni, kwa kweli tunajivunia maisha yake,” amesema Padri Matiika.

Related Posts