Dar es Salaam. Ununuzi wa taa za barabarani kutokana nje ya nchi huenda ukakoma, baada ya wataalamu nchini Tanzania kutengeneza taa za sola na umeme zenye uwezo wa kudumu miaka 100.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Julai 8, 2024 katika Maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Salome Lwanteze, mhandisi katika Kiwanda cha Sky Zone kinachomilikiwa na Suma JKT, amesema wameanza uundaji wa taa za sola na umeme za barabarani.
Amesema taa hizo zitapunguza changamoto za uwepo wa giza kwenye baadhi ya barabara na mitaa kwa wahitaji, hususani kwa mashirika binafsi na taasisi za Serikali.
“Taa tulizonazo zinatumika sehemu zote, ikiwepo kwenye viwanja vya michezo na tayari tumefunga kwenye Uwanja wa Uhuru na pia mitaani,” amesema Salome.
Hata hivyo, amesema kwa sasa wamejikita kwenye taa za sola kwa sababu hakuna kiwanda kinachotengeneza na wana uwezo wa kupima taa kwenye maabara zao, ili kusaidia wananchi kuhusu ubora wa taa kama zinapitisha maji au hazipitishi.
Si kwenye maji pekee, hata inapoanguka uharibikaji wake ni tofauti na nyingine na wametoa nafasi kwa mteja kueleza sifa ya taa anayohitaji kutengenezewa.
Msimamizi wa Idara ya Mipango na Usalama Barabarani wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Clever Akilimali amesema wanatamani anayetengeneza taa za sola awe na uhakika wa bidhaa yake, ili kuepuka matumizi ya muda mchache.
“Tanroads chini ya wizara kuna maelekezo tulipewa lazima tuweke ufafanuzi wa vigezo kwa sababu kila mmoja akienda analeta bidhaa na wakati mwingine wanaleta taa zinakaa muda mchache hazifanyi kazi,” amesema Akilimali.
Mkazi wa Goba, John Maige amesema kama maelezo yanayotolewa na wahusika yatakuwa na ukweli, itakuwa ni msaada kwa barabara zinazopita pembezoni mwa mjini ambapo kumekuwa na wimbo la matukio ya uhalifu.
“Kwetu Goba kunaonekana kama porini, husaani wakati wa usiku watu wanaogopa kutembea umbali mrefu kwa kuhofiwa kukabwa, Si tu barabara za mtaani hata barabarani kwenye magari mengi ni giza,” amesema Maige.
Amesema Serikali inatakiwa kukaa chini na Suma JKT na kuangalia namna watakavyoweza kukubaliana katika utengenezaji wa hizo na kufungwa kwenye barabara kubwa na ndogo, ikiwepo ya Morogoro.
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Rajabu Mabele ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la uzalishaji Mali la JKT (SUMAJKT), amesema uboreshwaji wa mazingira ya uwekezaji kumefanya Tanzania kuwa mahali salama pa kufanyia biashara.
“Tumeshiriki maonyesho haya mara nyingi na tumekuwa tukija na bidhaa bora, ili wananchi wapate kilicho bora na tunafanya biashara ambayo husaidia kuongeza uchumi wa nchi, kwani vifaa vyote mnavyoviona hapa tunalipa kodi na hili ni jambo la msingi sana,” amesema Mabele.
Pia, amesema wamekuwa wakishiriki maonyesho hadi ya nje ya nchi na wameshakwenda kwenye maonyesho Comoro na wakati mwingine watu wa mataifa ya nje wanakuja kufuata bidhaa za Suma JKT, Dar es Salaam.