Michango yamtoa gerezani aliyechoma picha ya Rais

Mbeya.  Siku nne tangu kijana Shadrack Chaula (24), aliyechoma picha ya Rais kuhukumiwa kulipa faini ya Sh5 milioni au kifungo cha miaka miwili, hatimaye michango ya wananchi imefanikiwa kumtoa katika Gereza la Ruanda Mkoa lililoko mkoani Mbeya.

Shadrack aliyekamatwa kwa madai ya kuchoma picha ya Rais Samia Suluhu Hassan na kushtakiwa kwa kosa la kutoa taarifa za uongo, alikwenda gerezani baada ya kushindwa kulipa faini hiyo.

Akizungumza leo Jumatatu Julai 8, 2024 baada ya kutoka katika Gereza la Ruanda akiwa ameambatana na wakili wake, Michael Mwangasa, kijana huyo ambaye ni Msanii wa Sanaana Uchoraji, amewashukuru Watanzania kwa kuchanga fedha na kumtoa gerezani.

“Nawashukuru Watanzania kwa upendo wa kunichangia fedha na mawakili mlionihangaikia kuja kunitoa gerezani wote nawaombea kwa Mungu awabariki sana,” amesema huku akiwa na uso wa furaha.

Kwa upande wake, wakili aliyekuwa akishughulikia suala hilo, Michael Mwangasa amesema wana nia ya kukata rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

“Hatujaridhika na hukumu iliyotolewa kwa sasa tunaweka mambo sawa hasa taratibu zote za kisheria kabla ya kwenda kukata rufaa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya,” amesema Mwangasa.

Kijana hiyo alipofikishwa mahakamani, alisomewa shitaka la kutoa na kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa TikTok, kosa ambalo ni kinyume cha sheria ya makosa ya mtandao kifungu cha 16.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya, Shamla Shehagilo, baada ya mshtakiwa huyo, mkazi wa Kijiji cha Ntokela, wilayani humo, kukiri kosa hilo.

Baada ya kukiri kosa hilo, Hakimu Shehagilo alimtia hatiani kwa kosa hilo na kumuhukumu kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela miaka miwili.

Awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Rosemary Mgenije, aliyekuwa akisaidiana na Wakili Veronica Mtafya, alidai Juni 22, 2024, eneo Ntokela lililopo Kata ya Ndato, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, mshtakiwa alitenda kosa hilo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii @jet.fightershop akiwa ameshika picha inayomwonyesha Rais Samia, akisema:

“Kwa kuwa umeshindwa kutetea Taifa lako lisiathirike na ushoga, hii video inakuhusu wewe na si mtu mwingine wakati ukijua taarifa hizo ni uongo na upotoshaji kwa jamii,” amedai Wakili Veronika.

Related Posts