VIJIJI 45 VYAWEKEWA MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI UVINZA

Na Munir Shemweta, WANMM UVINZA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amesema jumla ya vijiji 45 kati ya vijiji 61 katika wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma vimewekewa mipango ya matumizi ya ardhi.

Mhe. Pinda amesema hayo leo tarehe 8 Julai 2024 katika wilaya ya Uvinza wakati wa mwanzo wa ziara ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Isdori Mpanga mkoani Kigoma.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, mji wa Uvinza kwa sasa unakuwa kwa kasi na wizara yake kupitia Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo iliamua kuviwekea vijiji vya wilaya ya Uvinza Mipango ya Matumizi ya Ardhi ili kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile kilimo na ufugaji.

“Uamuzi wa kuviwekea mipango ya matumizi ya ardhi vijiji 45 katika wilaya ya Uvinza ni njia sahihi ya kupunguza mgongano wa matumizi ya ardhi na zoezi litaendelea katika vijiji vilivyobakia 16 ambavyo viko kwenye mpango kazi ” amesema Mhe. Pinda.

Mhe. Pinda alielezea pia mgogoro baina ya wananchi wa kijiji cha Mpeta na Ranchi ya NARCO, mgogoro uliosababishwa na wananchi wa kijiji hicho kutoridhika na hekta 2,500 walizopatiwa kutoka kipande cha ranchi ambapo kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi tayari serikali imesikia kilio cha wananchi hao na kuwapatia hekta nyingine 5,240 ili ziweze kutosheleza mahitaji.

Hata hivyo, amemtaka Mkuu wa wilaya ya Uvinza pamoja na mkurugenzi wa halmashauri kukaa na viongozi wengine wa wilaya hiyo kuhakikisha hekta zilizotolewa zinagawiwa kwa wananchi kwa lengo la kukidhi mahitaji.

Akikeukia mgogoro baina ya wilaya ya Kasulu na Uvinza kuhusiana na kitalu cha uwindaji alichopatiwa mwekezaji, Mhe. Pinda amemueleza Makamu wa Rais kuwa, kitalu alichopewa muwekezaji ramani yake ina mapungufu hivyo ameielekeza ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kigoma kukutana na halmashauri za wilaya husika husika ili kupata tafsiri sahihi ya ramani kwa lengo kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Isdori Mpango ameanza ziara yake mkoani Kigoma leo tarehe 8 Julai 2024 ambapo mbali na mambo mengine amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile umeme na barabara.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda (Kushoto) akuzungumza mbele ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philio Isdori Mpango wakati wa mwanzo wa ziara yake mkoani Kigoma tarehe 8 Julai 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akisisitiza jambo wakati wa mwanzo wa ziara ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philio Isdori mkoani Kigoma tarehe 8 Julai 2024.
Sehemu ya wananchi waliojitokeza wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Mpango tarehe 8 Julai 2024

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda (wa pili kulia) akiwa na baadhi ya mawaziri na viongozi wengine wa mkoa wa Kigoma wakimsikiliza Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Mpango (hayupo pichani) wakati wa mwanzo wa ziara yake mkoani Kigoma tarehe 8 Julai 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Related Posts