MAMLAKA Ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA,) imewataka wadau wa masoko ya mitaji kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwezesha wananchi kiuchumi na kutekeleza Mpango Kazi wa Serikali wa njia mbadala za kugharamia miradi ya maendeleo.
Hii itawezesha Serikali na Sekta Binafsi kupata rasilimali fedha za kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo, na kuchochea maendeleo ya kijamii na ukuaji wa nchini huku Mamlaka hiyo ikiendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuchagiza na kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.
Akizungumza Leo jijini Dar es katika hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Uwekezaji wa Pamoja wa kampuni ya Sanlam Investments East Africa Limited, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA,) CPA. Nicodemus Mkama amesema hiyo ni hatua muhimu katika maendeleo ya sekta ya fedha hususan masoko ya mitaji nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ameeleza kuwa, Aprili, 16 mwaka huu, CMSA iliidhinisha Waraka wa Matarajio (Offer Document) na Mkataba wa kuendesha Mifuko ya uwekezaji wa pamoja ya kampuni ya Sanlam Investments East Africa Limited yaani Sanlam Pesa Money Market Fund na Sanlam USD Fixed Income Fund Trust Deed.
“Idhini ilitolewa na CMSA baada ya Sanlam Investments East Africa Limited kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania; na Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya uanzishaji na uendeshaji wa Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja yaani “Capital Markets and Securities (Collective Investment Schemes), Regulations”. Napenda kuufahamisha umma kuwa, Sanlam Pesa Money Market Fund na Sanlam USD Fixed Income Fund ni mifuko ambayo imekidhi matakwa ya Sheria, Kanuni na Miongozo ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja.” Ameeleza.
Amesema kuwa lengo kuu la Mifuko hiyo ya Uwekezaji wa pamoja ni kuhamasisha wawekezaji wadogo, wa kati, na wakubwa kuunganisha nguvu zao na kuwekeza kwa pamoja ili kunufaika na fursa zinazopatikana katika sekta ya fedha, hususan masoko ya mitaji.
“Lengo mahsusi ya Mifuko hii ni kuwawezesha watanzania wa kada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake, makundi maalum, taasisi na mifuko ya hifadhi ya jamii kunufaika na uwekezaji unaosimamiwa na wataalamu waliopewa leseni ya kutoa huduma katika masoko ya mitaji; kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza; na kuwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za uchumi na kuongeza kipato.” Amefafanua.
CPA Mkama amesema kuwa Mamlaka hiyo ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli katika masoko ya mitaji zinafanyika kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta uwazi na haki kwa washiriki wote.
Aidha katika juhudi za kuwezesha kufikia malengo ya kuanzishwa kwa Mifuko hiyo CMSA imeidhinisha kushusha kiwango cha chini cha ushiriki katika uwekezaji kwenye Mifuko hiyo kutoka Shilingi milioni moja hadi Shilingi elfu 10 hatua itakayokuza ushiriki wa wawekezaji wa kada mbalimbali katika Mifuko hiyo, ikiwa ni pamoja na wananchi wenye vipato vya chini na vya kati.
Pia ameipongeza Bodi na Menejimenti ya Sanlam Investments East Africa Limited kwa kufanya uamuzi wa kufungua ofisi yao mpya jijini Dar es Salaam, Tanzania kwa ajili ya kutoa huduma ya usimamizi wa uwekezaji, hususan usimamizi wa mifuko yao ya uwekezaji na kueleza kuwa hiyo ni muhimu katika uwekezaji.
Masoko ya mitaji ni sehemu ya mfumo wa sekta ya fedha inayowezesha upatikanaji wa fedha za muda mrefu, yaani zaidi ya mwaka mmoja, kwa ajili ya kugharamia shughuli za maendeleo.
Fedha hizo hupatikana kwa kuuza hisa za kampuni, hatifungani za kampuni, hatifungani za taasisi, hatifungani za Serikali na vipande katika Mifuko ya Uwekezaji wa pamoja kutoka kwa wawekezaji, ambao ni watu binafsi, taasisi na kampuni na hatimaye fedha hizo huwekezwa katika sekta za uzalishaji na hivyo kuchochea ustawi na maendeleo ya uchumi.