Masharti mazito Simba… ulevi, fujo, jezi za Yanga marufuku

SIMBA ilipaa jana jioni kwenda Misri kujiandaa na msimu mpya wa 2024-2025 lakini siku moja kabla ya safari hiyo, wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi wakabebeshwa zigo na tajiri wa klabu hiyo akiwaambia salama yao iko hapo.

Pale pembeni kabisa ya Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam, Simba ilijifungia kwenye hoteli moja eneo la Mbezi Beach na kufanya kikao kizito kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘MO’ akiwa na viongozi wengine kuzungumza na mastaa wao. Kwenye mkutano huo wachezaji walikuwa wakitambulishwa juu ya timu hiyo na miiko mbalimbali inayoihusu.

Ndani ya mkutano huo, wachezaji na benchi la ufundi chini ya kocha mkuu mpya, Fadlu Davids walibebeshwa malengo ya klabu kwa msimu ujao ni kwamba wanapaswa kuhakikisha wanabeba Kombe la Shirikisho Afrika.

Kama sio kombe hilo, basi kikosi hicho kinatakiwa kutinga fainali ya michuano hiyo ili kutuliza presha ya mashabiki baada ya kushindwa kufikia malengo katika misimu mitatu iliyopita.

Ukiacha lengo la kimataifa, pia vigogo waliwataka mastaa kujiweka kando na kejeli za watani wao Yanga kwa kuanzia watetee Ngao ya Jamii waliyoibeba msimu uliopita walipoifunga Yanga kwa penalti.

Mbali na Ngao ya Jamii, pia wanatakiwa kuchukua Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho (FA), mataji ambayo Yanga imeyachukua mara tatu mfululizo.

Katika mkutano huo pia wachezaji waliambiwa ni marufuku kuvaa nguo ambazo hazitakiwi kuzivaa wakiwa Simba na kwamba nguo yoyote inayoashiria rangi ya jezi zinazotumiwa na watani wao ni marufuku kuvaliwa kambini au nje ya kambi. Nguo rasmi za kuvaa wakati wakiwa kambini ni zenye nembo ya wadhamini na ile ya klabu, hivyo atakayekutwa amekiuka utaratibu atajiingiza matatizoni.

“Hatutakiwi hata kuvaa jezi za Yanga tukibadilishana na wenzetu wa kule na kama ukitokea umebadilishana na mwenzako, unatakiwa kuishika na kwenda kuitunza ndani kwako na sio kuivaa pale uwanjani. Lazima kila mchezaji azilinde nembo za klabu pamoja na wadhamini,” alisema nyota mmoja wa Simba.

Wachezaji pia walitangaziwa kwamba meneja mpya wa timu hiyo atakabidhiwa kifaa maalumu kitakachotumika kupima kama mchezaji ataingia kambini amelewa ambapo kama atakuwa amekunywa atazuiwa na kukumbana na adhabu.

Mbali na hayo wachezaji walielezwa kuwa wanatakiwa kufuata utaratibu ambao utawekwa na meneja wa timu hiyo kambini na ndiye ataombwa ruhusa mchezaji anayetaka kutoka nje kwani ndiye ataulizwa endapo kuna mchezaji atakuwa haonekani.

Pia walielezwa kuwa pamoja na kwamba utaratibu mwingine utawekwa, lakini walikumbushwa kuuheshimu muda wa kula na ukifika kila mmoja awe amekaa mezani bila udhuru.

Vilevile walielezwa kuhusu muda wa kwenda kwenye gari wakati timu inakwenda mazoezini au mechi kuwa kila mmoja anatakiwa kufika kwa wakati na kuondoka uwanjani kwa wakati na pia wamepigwa marufuku kuongea na waandishi wa habari bila idhini ya meneja.

Timu hiyo iliondoka jana ikiwa na wachezaji 30 chini ya kocha msaidizi Seleman Matola, kwenda nchini Misri.

Wachezaji ambao Simba haijaondoka nao ni Sadio Kannoute, Pa Omar Jobe, Babacar Sarr ambao wanafanya mazungumzo namna ya kumalizana nao kutokana na mikataba waliyo nayo, huku kipa Atoub Lakred akitarajiwa kuungana na timu Misri.

Related Posts