KAKOLANYA: Chama? Subirini mtaiona Yanga

MASTAA kung’oka kutoka Simba kwenda Yanga imekuwa hali ya kawaida na inaendelea kufanyika mwaka hadi mwaka, na mojawapo ya sajili za aina hiyo zilizotingisha ilikuwa ni Haruna Niyonzima kusajiliwa na Simba akitokea Yanga.

Usajili huo uliwachefua mashabiki wa Yanga hadi kufikia hatua ya kuchoma jezi ya staa huyo wa Rwanda, wakiamini kwamba hakuwatendea haki bila kujali kuwa yeye pia ni binadamu anatafuta maslahi yake na familia.

Uhamisho wa Bernard Morrson ambaye pia alitimkia Simba akitokea Yanga pia ulitingisha na maneno mengi yalizungumzwa, lakini baadaye alirudi tena Jangwani na mambo mengine yaliendelea.

Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza na staa aliyepita katika timu hizo mbili zenye upinzani wa jadi, Beno Kakolanya ambaye amefunguka mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuzungumzia dili la msimu huu la Clatous Chama kutua Yanga akitokea Simba.

“Chama ni mchezaji anayejielewa, ana kila kitu, kuhamia upande wa pili anatakiwa kutengenezwa kisaikolojia tu, sina shaka naye. Ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na anaweza kufanya kitu bora msimu ujao,” anasema Kakolanya.

“Wengi wanaamini mchezaji akitoka timu moja kwenda nyingine hasa Simba na Yanga anaweza kufanya vibaya, lakini kwa uwezo wa Chama naona akiwa bora.”

Wakati stori ya mjini ikiendelea kuwa ni usajili wa Chama kutua Yanga akitokea Simba, Kakolanya anasema habari hiyo haijamshangaza kwasababu mpira ni biashara.

“Chama kuondoka Simba hakuna mtu alikuwa anatarajia lakini kwa sisi wachezaji tunachukulia kawaida kwani ni biashara yetu, maisha ndio yanatufanya tuwe hivyo,” anasema kipa huyo.

“Mfano hata mimi kuondoka Simba ni kwa sababu ya maslahi sikuondoka kwa ubaya, natumaini hilo pia limetokea kwa Chama asingeweza kuondoka kama makubaliano ya maslahi yalikwenda vizuri amefanya hivyo kwa sababu ya kutafuta fedha.”

Kipa huyo wa zamani wa Yanga, Simba, Singida Big Stars na Tanzania Prisons, anasema wachezaji wanatafuta maisha, ndio maana leo wanaweza kucheza timu hii na kesho wakawa kwingine na anaamini Simba inataka kuja tofauti ndio maana inajisuka upya.

Wakati inaelezwa kuwa huenda Manula asiwe sehemu ya kikosi cha Simba msimu ujao, Kakolanya anamkingia kifua kuwa bado ana nafasi ya kuendelea kuitumikia timu hiyo, ila majeraha ndio yaliyomrudisha nyuma.

“Bado ni mchezaji mzuri na namtarajia akiwa bora msimu ujao kwani tayari ameshaanza kufanya mazoezi na amerudi kwenye utimamu. Kuhusu Manula kuondoka Simba siwezi kuthibitisha hilo, ila naamini bado ni mchezaji wa timu hiyo na ana nafasi ya kufanya vizuri,” anasema.

“Nimesikia tu kwenye mitandao kuwa anakwenda kwa mkopo Azam FC, sina uhakika na sizipi sana nafasi stori za mitandaoni, naamini Aishi bado ni mchezaji wa Simba na atakuwa bora zaidi.”

Inaelezwa kuwa kinachomponza Kakolanya hadi kumalizana vibaya na timu alizozitumikia ni tabia ya ujeuri aliyonayo, lakini mwenyewe amelikana hilo huku akithibitisha kuwa misimamo yake ndiyo inayomponza.

“Mimi sio mkorofi ni mtu wa watu, asiyenifahamu nje ya mpira hawezi kunielewa, kwa ishu zinazotokea dhidi yangu kwenye masuala ya mpira zinatokana na misimamo yangu na hiyo ndiyo inanifanya nionekane mtovu wa nidhamu,” anasema na kuongeza;

“Ukiona timu inanitaja kwenye utovu wa nidhamu basi ujue nimesimama kwenye haki, lakini sipo hivyo mbona Simba nimeishi vizuri miaka minne nimeondoka vizuri, Tanzania Prisons miaka mitatu pia nimeondoka vizuri lakini mimi ni mtu ambaye napenda kusimama kwenye haki hasa kwenye kazi yangu ya mpira lakini sio mkorofi.”

Kakolanya amesema dunia ina mambo ya kushangaza na ukitaka kuonekana mkorofi, dai chako.

“Ndio nikiwa Yanga nilimaliza kwa madai ambayo nashukuru Mungu haki yangu ilipatikana hivyo naamini maisha kama haya ninayoyapitia yapo sana kwenye mpira na nimekuwa nikijifunza kwa wengine yakinipata nafanya kwa uelewa,” anasema.

MAKIPA WAGENI BORA ILA KUNA YONA

Wakati wadau wakilia na makipa wazawa kushindwa kufanya vizuri mbele ya makipa wageni akiwemo Djigui Diarra wa Yanga, Kakolanya amekiri kweli ubora wa wageni umekuwa mkubwa lakini amemtaja Yona Amosi kuwa anaibuka na ubora.

“Ni kweli kuna haja ya kuongeza nguvu eneo hilo kwasababu kuna changamoto ya wageni kufanya vizuri japo sio wote kwani kuna ambao kiwango chao kipo chini, nafikiri pia kwa upande wa wazawa kuna makipa wanaochipukia na wako vizuri,” anasema na kuongeza;

“Mfano mzuri ni Yona Amosi wa Tanzania Prisons, ni kipa ambaye anachipukia, amepandishwa kutoka timu ya vijana, amecheza vizuri msimu ulioisha na pia kuna kipa wa Geita Gold kapandishwa na kaonyesha uwezo.”

Kakolanya amesema hata kwa upande wao makipa wazoefu wana kazi ya kufanya kuhakikisha wanaongeza ubora ili kuonyesha ushindani kwa wageni.

Kakolanya amecheza timu mbili za Kariakoo, Simba na Yanga, na kutoka kwenda kujaribu maisha mengine nje ya timu hizo.

Amefunguka kuwa anafahamu mazuri na mabaya ya kucheza huko lakini sasa amesahau na anafurahia maisha ya timu aliyopo.

“Mimi nimeanzia chini na kupanda juu, hivyo kucheza Simba na Yanga nafahamu maisha ya huko. Siwezi kurudi huko  kwa sasa kwasababu tayari ni maisha ambayo yameshapita, nilipo sasa nafurahia maisha niliyonayo na huwa nayapa kipaumbele.”

Msimu uliopita kulikuwa na bato la ushindani kuwania tuzo ya mfungaji bora, ikiwa kati ya viungo wawili kutoka Yanga na Azam FC, Stephane Aziz Ki na Feisal Salum ‘Fei Toto’. Kakolanya ametaja sababu anayoamini ilimfanya Ki kuibuka mfungaji bora kuwa ni umoja wa timu yake.

“Timu nzima ya Yanga ilikuwa inampambania Aziz Ki kwa kumtengenezea mazingira mazuri ya kufunga wakati kwa upande wa Fei Toto timu yake ilikuwa inapambania nafasi ya pili hii ndio changamoto iliyo muangusha,” anasema na kuongeza;

“Bato lilikuwa ni zuri na gumu lakini mwisho wa yote aliyekuwa anatengenezewa na wenzake ameibuka shujaa na mechi ya mwisho ndio iliamua hii ilileta msisimko kwenye ligi.”

Kakolanya anasema Azam FC walitakiwa kumtengenezea Fei Toto zaidi kama ilivyokuwa kwa Aziz Ki na wachezaji wenzake lakini anaamini ilichangiwa na kutafuta nafasi ya pili ambayo walifanikiwa kuipata.

Licha ya kutajwa kutua JKT Tanzania, nahodha wa zamani wa Simba, John Bocco amesomea ukocha na tayari amefanya kwa vitendo akiwa na kikosi cha vijana cha Simba na Kakolanya amezungumzia namna alivyoshawishiwa na mshambuliaji huyo kusomea ukocha.

“Mwanzo nilikuwa sitamani kabisa kuingia huko lakini Bocco siku moja aliniambia ‘Beno unaweza kufundisha, usiache kufanya hili.’ Ndio maana nimeliweka jambo hili kwenye mipango yangu, ipo siku nitalifanya,” anasema na kuongeza;

“Nikiwa naendelea kucheza nitajaribu kusomea ukocha na muda ukifika nitaingia huko kwenye kufundisha makipa kwasababu ndio kazi ninayoitumikia sasa.”

JERAHA TATA YANGA, PRISONS

Kwenye maisha ya mwanadamu kila mmoja amepitia changamoto ambazo kwa namna moja ama nyingine zilikaribia kumkatisha tamaa iwe kwenye masomo, kazi au mishe nyingine.

Beno amekiri kuwa ameshawahi kukutana na majeraha kwenye kazi yake ambayo aliamini mpira kwake basi.

“Nakumbuka nikiwa Tanzania Prisons nilipata jeraha la pega ambalo licha ya kwenda hospitalini na kupiga mionzi (X Rays) ili nifahamu shida ni nini lakini sikuwa naona tatizo nilikaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu na nilikuwa nasikia maumivu makali licha ya kutokubainika kwa shida yangu ilikuwa ni nini,” anasema na kuongeza;

“Shida nyingine niliipata nikiwa Yanga nilikaa nje ya uwanja mwaka mzima, nakumbuka nilicheza mechi mbili au tatu msimu mzima shida ilikuwa ni goti lakini nashukuru Mungu pia nilipata dawa na kurudi kwenye hali yangu ya kawaida hadi sasa nipo fiti,” anasema.

Related Posts