Namna makachero walivyomdaka mwizi wa bastola

Moshi. Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Benedicto Petro aliyeongoza timu ya makachero kuwakamata washtakiwa wa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, ameeleza namna walivyomkamata mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Eben Mwaipopo.

Mshitakiwa huyo alikamatwa katika Kituo cha Basi cha Bomang’ombe wilayani Hai.

 Shahidi ameeleza kuwa, katika mahojiano,  mshitakiwa aliwaeleza alipoificha silaha iliyotumika katika mauaji mkoani Tanga, ambayo baadaye ilibainika iliibwa mjini Moshi.

Mwaipopo (27) ambaye kwa jina maarufu Hashim na mwenzake, Fredrick Mkweme au white, wanakabiliwa na makosa mawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kukutwa na mali inayosadikiwa kuwa ya wizi, kinyume cha sheria.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuiba bastola aina ya Norinco yenye thamani ya Sh350,000, risasi 27 za Sh75,600, Paundi 30,000(Sh79.6 milioni)  na mashine ya kupima damu yenye thamani ya Sh100,000.

Kulingana na hati ya mashitaka, wawili hao wanadaiwa kuiba televisheni moja yenye thamani ya Sh1.2milioni mali ya Denis Swai pamoja na kuwaweka chini ya ulinzi watu wawili Idda Swai na Daniel Shayo na kuchukua mali hizo.

Akitoa ushahidi wake katika Mahakama ya Wilaya ya Moshi, Benedicto amedai Mwaipopo alikamatwa na maofisa wa polisi Januari 25 mwaka 2018 na kupelekwa Tanga alikokuwa akikabiliwa na shtaka la mauaji ya kukusudia.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, baada ya kuhojiwa Tanga,  mshitakiwa aliwaeleza silaha  iliyotumika iko Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha.

Shahidi ameeleza kuwa, Mwaipopo alikamatwa na maofisa wa polisi katika Kituo cha Basi cha Bomang’ombe, Wilaya ya Hai, Januari 25 2018.

 Shahidi huyo amedai kuwa, Machi 1, 2018 akiwa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO), Mkoa wa Tanga, aliagizwa na RCO kuanza safari kwenda kuitafuta iliko silaha hiyo, na waliikuta kwenye begi la mshtakiwa wa kwanza kwenye chumba alichodai kupewa na shemeji yake, Ritha Makule.

Akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Kambarage Samson mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Moshi, Ruth Mkisi, Shahidi huyo amedai kuwa, washtakiwa hao walichukuliwa na maofisa wa Polisi Kilimanjaro kutoka Tanga, Juni 6 mwaka 2022.

Aliieleza Mahakama hiyo kuwa, waliarifiwa na Polisi Kilimanjaro kwamba, washtakiwa hao walikuwa wakituhumiwa kuhusika katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Katika ushahidi wake alidai mtaalamu wa milipuko, alipoifanyia uchunguzi bastola aina ya Norinco yenye namba za usajili 47012895, rangi nyeusi, alibaini silaha hiyo inamilikiwa na Swai na iliibwa Juni 28, 2017 eneo la Soweto, Moshi.

Amedai kuwa, walipofanya upekuzi waligundua bastola hiyo haikuwa na magazine.

Wakati mshtakiwa wa pili, Fredrick Mkweme (White), alikamatwa Januari 27 mwaka 2018 akiwa katika shughuli zake za bodaboda eneo la Bonite, Moshi.

Baada ya kutoa ushahidi huo,kuliibuka mabishano ya kisheria kati ya Mwaipopo na shahidi.

Mwaipopo alitaka Mahakama iruhusu apewe maelezo ya shahidi ili ayatumie kumdodosa shahidi huyo kuhusiana na kile alichoieleza.

Kutokana na mvutano huo, Hakimu Mkisi, aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 6 mwaka huu, Mahakama itakapotoa uamuzi wake kuhusu mapingamizi yaliyojitokeza na baada ya uamuzi huo mdogo, kesi hiyo itaendelea kwa mashahidi kuendelea kutoa ushahidi.

Related Posts