SIMBA huenda ikamtoa kwa mkopo beki wake wa kulia, David Kameta ‘Duchu’ baada ya kushindwa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo kwa msimu uliopita.
Inaelezwa kwamba Simba na Duchu wapo kwenye mazungumzo na timu nyingine za Ligi Kuu Bara ili kumpeleka beki huyo ambaye awali alitua kikosini hapo Agosti 2020 akitokea Lipuli ya Iringa.
Katika eneo lake ndani ya Simba amekuwa akicheza Shomari Kapombe na wakati mwingine Israel Mwenda, huku yeye akisugua benchi.
Hata hivyo zipo timu tatu ambazo zinatajwa kwa sasa kumtaka mchezaji huyo, ikiwamo Pamba Jiji ambayo imepanda msimu huu ikitokea Championship msimu uliopita.
Timu nyingine ni KenGold na Singida Fountain Gate, lakini hadi jana asubuhi kulikuwa hakuna ambayo ilikuwa imemalizana na Simba wala mchezaji huyo.