Tabora. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepata pigo baada ya makada wake wawili akiwemo katibu wa chama hicho Wilaya ya Tabora Mjini, Maxmilliani Jerome kutimkia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katibu huyo wa Chadema amekikacha chama hicho cha upinzani nchini Tanzania kwenda chama tawala ikiwa ni wiki moja tangu aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa atimkie CCM.
Mbali na Maxmilliani, mwanachama mwingine wa Chadema aliyejiunga CCM mkoani humo katika mapokezi yaliyofanyika viwanja vya TBC Manispaa ya Tabora ni aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Filta kwa tiketi ya Chadema, Richard Rite.
Wanachama hao wapya wamepokewa jana Jumatatu Julai 8, 2024, na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Said Nkumba ambaye alichaguliwa katika nafasi hiyo Julai 5, mwaka huu kwa kura 1,006 kati ya 1,119 kujaza nafasi ya Hassan Wakasuvi aliyefariki Februari 22, 2024.
Kwa mujibu wa Nkumba, kazi yake katika wadhifa huo ndiyo imeanza huku akiahidi Wanaccm wajipange kuendelea kuvuna wanachama wapya hususan kutoka vyama vya upinzani.
“Kwa mujibu wa Katiba ya CCM inaturuhusu kupokea wanachama wapya kwa lengo la kujiongezea nguvu kwenye chama. Tunao mkakati wa kuendelea kupokea wanachama wengi zaidi kwa lengo la kukijenga chama chetu,” amesema Nkumba.
Mwananchi Digital imemtafuta, Maxmillian Jerome kujua kilichomsukuma kutimkia chama tawala, ambapo ametaja sera na uwazi uliopo ndani ya chama hicho kuwa kivutio kwake.
“Binafsi nimevutiwa na utendaji kazi wa Chama cha Mapinduzi ndiyo maana nimeamua kujiunga na chama hiki, yako mengi ambayo yamenivutia lakini kikubwa nimekuja kuongeza nguvu kuhakikisha chama hiki kinaendelea kushika dola na sitakuwa msaliti kamwe.”
“Nilikuwa kiongozi ambaye nilikuwa naongoza kata 29 katika wilaya hii ya Tabora kwa hivyo huu mji naufahamu vizuri kwahivyo ninawaomba mnitumie na nitakuwa pamoja nanyi katika kuhakikisha tunashinda chaguzi zote zilizoko mbele yetu ili tuendelee kushika dola,” amesema Jerome.
Mwananchi haikufanikiwa kumpata Richard Rite ziligonga mwamba baada kumsaka bila mafanikio kujua kilichomsukuma kufikia uamuzi huo.