Arusha. Mahakama ya rufani imetengua hukumu ya kifungo cha maisha jela, aliyohukumiwa Emanuel Samwel, baada ya kukutwa na hatia katika makosa ya ulawiti na ubakaji.
Hiyo ni baada ya kubaini kwamba Mahakama ilikosea kumtia hatiani kijana huyo pasipo kuthibitisha kwamba alikuwa mtu mzima.
Kutokana na usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo kutokuelezwa endapo mrufani alikuwa na umri wa miaka 18 wakati anatenda makosa hayo, mahakama imesema hukumu iliyotolewa ya kifungo cha maisha ni kinyume cha sheria.
Rufaa hiyo namba 304/2021 inatokana na uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara ya Machi 12, 2021 katika rufaa ya jinai namba 22/2020.
Hukumu hiyo ilitolewa Juni 5, 2024 na Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Stella Mugasha, Dk Mary Levir na Omary Othman Makungu.
Awali mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Manyara, mrufani alisomewa mashitaka ya ubakaji na ulawiti kinyume na kifungu cha 130 (1) (2) (e), 131 (1) na (3), na 154 (1) (a) cha Kanuni ya Adhabu.
Ilidaiwa Julai 16, 2018 katika Kijiji cha Maganjwa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Emmanuel alimbaka na kumlawiti mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane.
Baada ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, mrufani Emmanuel alitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa yote mawili na adhabu ya viboko vitatu.
Hivyo alikata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambako kesi hiyo ilisikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi iliyokuwa imepewa mamlaka ya kuisikiliza rufaa hiyo, ambayo ilithibitisha adhabu iliyokuwa imetolewa na mahakama ya chini.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa siku ya tukio mwathirika wa tukio hilo saa 12 jioni alitumwa kwenda mashine ya kusaga, akiwa njiani alikutana na Emmanuel ambaye alimbeba hadi kwenye mashamba ya shule na kumlawiti. Ilidaiwa kuwa mwathirika huyo alipata majeraha katika sehemu zake za siri huku eneo la haja kubwa likitoa damu na alipoulizwa alimtaja mrufani kuhusika na tukio hilo.
Julai 7, 2018 shauri hilo liliripotiwa polisi kisha mtoto huyo akapelekwa hospitalini na alishonwa sehemu zake za siri kutokana na sehemu hizo kuchanika.
Mrufani alikana kutenda makosa hayo na kudai siku ya tukio alishinda shambani siku nzima kwa kuwa alikuwa na kazi nyingi huko usiku ndipo alikamatwa na kiongozi wa nyumba kumi.
Alivyokata rufaa Katika hati yake ya rufaa ya Machi 27, 2023, mrufani huyo alikuwa na hoja nane ambazo ni pamoja na mahakama ya awali ilikosea kisheria kumhukumu akidai hati ya mashtaka ilikuwa na dosari isiyoweza kuthibitika kwa kutaja kifungu cha 131(1)(e) ambacho hakipo kwenye Kanuni ya Adhabu.
Nyingine ni Mahakama ya kwanza ya rufaa ilikosea kisheria kwa kutoona kwamba umri wa wake ulikuwa chini ya miaka 18 wakati wa kutenda kosa hilo, hivyo, kukiuka kifungu cha 160B cha Kanuni ya Adhabu.
Hoja nyingine ni Mahakama ya Rufaa ya kwanza ilikosea kuthibitisha hukumu hiyo kutokana na ushahidi wa shahidi wa tatu ambaye alidai kuwa mrufani alikiri kutenda kosa ila alishindwa kutoa maelezo hayo ya onyo.
Pia, Mahakama ya kwanza ya rufaa ilikosea kisheria kwa kutoona kuwa shahidi wa kwanza alishindwa kupiga mayowe kuomba msaada wakati mrufani alipokuwa akimbaka, hivyo inaashiria kuwa kesi hii ilitengenezwa dhidi yake.
Nyingine ni mahakama ilikosea kisheria kwa kutozingatia ushahidi wa utetezi wa mrufani na mahakama hiyo kukosea kisheria kwa kutoona kuwa mrufani alinyimwa haki yake ya kuwakilishwa na wakili kinyume na kifungu cha 310 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Aidha, Juni 26, 2024, aliwasilisha hoja za nyongeza katika rufaa hiyo, mjibu rufaa aliwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Naomi Mollel, waliopinga hoja hizo na kuomba mahakama itupilie mbali rufaa hiyo.
Huku akinukuu mashauri mbalimbali, Jaji Stella Mugasha amesema kila shahidi anayo stahiki ya kuthibitishwa na lazima aaminiwe na ushuhuda wake kukubaliwa isipokuwa kama kuna sababu nzuri na za msingi za kutomwamini shahidi.
Alisema katika kesi ya sasa, mwathirika alisimulia jinsi alivyodhalilishwa na mrufani siku ya tukio na kumtaja kwa mama yake na kiongozi wa nyumba kumi, ushahidi uliofanikisha kumkamata mwathirika.
Jaji Mugasha amesema maelezo yaliyotolewa na daktari aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo, yalithibitisha kuwa ni kweli mwathirika alibakwa na kulawitiwa.
Hata hivyo, amesema jopo hilo la majaji wameridhika kuwa mashahidi wa upande wa mashtaka walitoa maelezo ya kuaminika juu ya kutokea kwa tukio hilo.
Kuhusu malalamiko ya mrufani kuwa utetezi wake haukuzingatiwa;
Amesema baada ya kupitia hoja za pande zote wamejiridhisha kuwa mahakama za chini zilizingatia ushahidi wa mrufani ambaye alijitetea na ushahidi wa mashtaka ulithibitisha alimbaka na kumlawiti mwathirika huyo.
Kuhusu ushahidi wa mwathirika kuchukuliwa, amesema ushahidi wa mashahidi wenye umri mdogo unadhibitiwa na masharti ya kifungu cha 127 (2) cha Sheria ya Ushahidi na kuwa baada ya kupitia mwenendo wa kesi hiyo, wamebaini hakuna sheria iliyovunjwa wakati anatoa ushahidi wake.
Kuhusu kunyimwa haki ya kuwakilishwa na wakili, Jaji Mugasha alisema kifungu cha 310 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinatoa haki ya uwakilishi wa kisheria, lakini haihitaji kwamba mshtakiwa lazima afahamishwe haki hiyo.
Amesema Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019 haihitaji kwa lazima kwamba mshtakiwa lazima afahamishwe kuhusu haki hiyo na kuwa katika kesi hiyo mrufani hakuwahi kuonesha kwamba angependa kuwakilishwa na wakili.
Akinukuu kesi ya rufaa ya jinai namba 144/2017 iliyofunguliwa na Maganga Udugali dhidi ya Jamhuri, mahakama ilieleza kuwa: “…hawezi kulalamika kwamba alinyimwa haki ya uwakilishi wa kisheria ambapo haimo kwenye kumbukumbu kwamba alieleza matakwa yake ya kuwa na uwakilishi wa kisheria na kwamba mahakama ya mwanzo kwa namna yoyote ile, ilimkataa au kumzuia kufanya hivyo. kufurahia haki.”
Jaji huyo amesema katika kesi hiyo mrufani alipewa haki kwa kusomewa mashtaka na kuelezwa kwa lugha anayoielewa, alielekezwa kuchagua namna ya kutoa utetezi wake alioutumia na kuleta mashahidi watatu waliotoa ushahidi wa upande wa utetezi.
“Katika mazingira hayo, hakuna kushindwa kwa haki kulikotokea kwa upande wa mrufani na hivyo malalamiko katika msingi wa nane hayana msingi. Katika mazingira hayo, makosa mawili ya ubakaji na ulawiti yalithibitishwa na mrufani alitiwa hatiani ipasavyo,” amesema.
Kuhusu hoja ya umri wa mrufani wakati anahukumiwa, amesema imeamriwa kuwa mahakama ya rufaa inaweza kubadilisha au kuingilia hukumu iliyotolewa na mahakama za chini ambapo kuna sababu za kufanya hivyo ikiwa ni pamoja na pale ambapo hukumu iliyotolewa ni kinyume cha sheria.
Hivyo Jaji Mugasha amesema suala hilo limesisitizwa katika matukio kadhaa huku wakinukuu mashauri yaliyowahi kutolewa maamuzi na mahakama ya rufaa.
“Katika kesi ya sasa, kwa kuwa wakati wa usikilizwaji wa awali na kesi haikubishaniwa kuwa mrufani alikuwa na miaka 18 wakati wa kutenda kosa hilo, hukumu iliyotolewa ya kifungo cha maisha ni kinyume cha sheria,” amesema.
“Tunasema hivyo kwa sababu kifungu cha 160B cha Kanuni ya Adhabu kinakataza hukumu za namna hii kwa mtu aliye chini ya miaka 18.
Kwa kuzingatia msimamo huo wa sheria, haikuwa sahihi kumhukumu mrufani kifungo cha maisha jela na kuongeza viboko vitatu vya fimbo,” amesema Jaji Mugasha.
Alihitimisha kwa kubatilisha hukumu zilizotolewa kwa mrufani na kuruhusu rufaa na kuagiza mrufani kuachiwa huru.