CCM Iringa wampokea Msingwa rasmi

Iringa. Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa mjini kimempokea aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, aliyejiunga na chama hicho hivi karibuni huku wakiahidi kumpa ushirikiano.

Chama hicho kimeahidi kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu mbalimbali ndani ya chama hicho kama mwanachama mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Julai, 2024,  katika ofisi za CCM Wilaya ya Iringa, Katibu wa chama hicho, Hassan Makoba amesema wanamkaribisha Msigwa kwa mikono miwili na kitampa ushirikiano wa dhati katika kazi za chama.

Makoba amesema; “Tutaendelea kushirikiana naye katika kutekeleza majukumu ya chama na kuhakikisha tunaleta maendeleo kwa wananchi wilayani hapa na mkoa kwa ujumla.”

Mchungaji Msigwa amesema  kazi iliyombele yake kwa sasa ni kusaidia kueneza mazuri yote yanayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Msigwa alisisitiza kuwa ataelekeza nguvu zake katika kusaidia kutekeleza mipango na sera za chama ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla.

Mchungaji Msigwa kwa mara ya kwanza alitangazwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika Jumapili Juni 30, 2024 kuwa amekihama chama chake cha Chadema na kujiunga rasmi na chama hicho.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi ndiye aliyemshika mkono Mchungaji Msigwa na kuingia naye ukumbini kulikokuwa na wajumbe wa NEC, ambao walimshangilia kwa makofi na nderemo.

Hata hivyo, itakumbukwa Mei 29, 2024, Mchungaji Msigwa ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini, alishindwa kutetea nafasi ya uenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa baada ya kubwagwa na Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu kwa tofauti ya kura mbili.

Hata hivyo, baada ya kushindwa uchaguzi huo, Mchungaji Msigwa aliyewahi pia kuwa kada wa NCCR-Mageuzi alisema ataendelea kukitumikia Chadema huku akisema hakujiunga na chama hicho kwa ajili ya uongozi na aliahidi kumpa ushirikiano Sugu.

Related Posts