Hemed: Wazanzibari badilisheni mitazamo kazi za hotelini

Unguja. Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla, amesema licha ya kuwapo malalamiko kuwa kazi za hoteli kisiwani humo zinatolewa kwa wageni, changamoto ipo kwa wazawa kutothamini kazi hiyo, hivyo kuwataka wabadilishe mitazamo yao.

Amesema kazi za hoteli na sekta ya utalii zinahitaji kujituma, hivyo wanaopata bahati kuajiriwa, wazingatie utoaji wa huduma bora.

Hemed ametoa kauli hiyo wakati akiwatunuku vyeti wahitimu wa Chuo cha Mafunzo ya Utalii (ZCET) leo Jumanne, Julai 9, 2024, Michamvi Mkoa wa Kusini Unguja, huku akiwasisitiza kufanya kazi kwa bidii.

Makamu wa Pili amesema kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mengi kwamba asilimia kubwa ya kazi za hoteli zinachukuliwa na wageni kutoka nje, lakini hilo linasababishwa na wazawa wenyewe kutokuthamini ajira wanazopata.

Amesema wakati wote wamiliki huangalia zaidi sifa na vigezo, ikiwemo kuheshimu miongozo na uwajibikaji badala ya kukwepa majukumu hata pale isipokuwa lazima.

“Vijana wengi wa Zanzibar na Tanzania wamebahatika kusafiri na kufanya kazi mbalimbali nje ya nchi, lakini misingi ya huko ni kufuata utaratibu, nidhamu, maadili na kujali wakati. Lazima uingie na kutoka kazini kwa muda unaotakiwa vinginevyo utaharibikiwa,” amesisitiza.

Hata hivyo, amesema ingawa katika ubinadamu dharura kama za misiba na harusi zinakubalika, lakini baadhi ya watu hutumia fursa hiyo kuondoka kazini na kwenda kufanya mambo yao mengine.

Amesema pasipokuwa na nidhamu kazini, ni vigumu kufanikiwa na waajiri wataendelea kutoa nafasi za ajira kwa watu ambao kweli wanataka kazi.

“Tuache tabia ya kutoheshimu misingi ya kazi tunazopata, mkifanya hivyo daima mtafanikiwa hata kupata ajira nje ya nchi kama Dubai, Canada na kwengineko na kuitangaza vyema Zanzibar na Tanzania,” ameeleza Hemed.

Kwa upande mwengine, Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuimarisha mazingira mazuri katika uwekezaji, ili kuvitangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyosheheni nchini.

Amesema juhudi za Serikali zimewezesha kupiga hatua kubwa ya uwekezaji kwenye sekta ya utalii na sasa Zanzibar ina takriban hoteli 700 za hadhi mbalimbali, hali inayoongeza idadi ya watalii na kuinua pato la Taifa.

Awali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohammed Mussa, amesema Serikali inathamini mchango na ushirikiano katika kuhakikisha mradi wa mafunzo ya amali kwa vijana 250 unafanikiwa, ili kuwapa stadi za maisha zitakazowafanya wakubalike kwenye soko la ajira.

Ameuomba uongozi wa Chuo cha Mafunzo ya Utalii kuwafunza wanafunzi kuzingatia maadili na utamaduni wa Mzanzibari hasa katika mavazi, mapishi na staha katika kuwahudumia wageni.

Naye Taufiq Salum Tourky, mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho amesema dhamira yao ni kuwawezesha vijana kwa kuwapa ujuzi na njia ya kuondokana na ukosefu wa ajira.

Amesema uamuzi wa kuanzisha chuo hicho umetokana na ukweli kwamba asilimia 60 ya kazi za kitalii zinashikwa na watu kutoka nje, wakati Zanzibar ina fursa nyingi ambazo vijana wakiwezeshwa wataweza kunufaika nazo. 

Naye Mwakilishi Mkaazi wa Unicef nchini, Laksin Bawani ameahidi shirika hilo kwa kushirikiana na Global Affairs Canada litaendelea kutoa msaada wa kiufundi na kifedha, ili kuhakikisha vijana wakiwemo wasichana wadogo wanapata mafunzo stahiki, ili kufikia malengo ya kujiinua kimaisha na kiuchumi.

Jumla ya wahitimu 90 walitunukiwa vyeti baada ya kuhitimu mafunzo ya miezi tisa yanayohusu idara mbalimbali za hoteli na utalii.

Related Posts