Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewataka vijana na kina mama kushiriki katika kudhibiti na kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa pindi wagombea wanapowashawishi wawachaguliwe kwa kutoa rushwa.
Akizungumzia leo Jumanne, Julai 9,2024 kuhusu udhibiti wa vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi katika Kipindi cha Elimu Jamii cha Redio Maria kutoka makao makuu Dodoma, Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa Takukuru, Joseph Mwaiswelo amesema vijana wanatakiwa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili Taifa lipate viongozi bora.
Amesema mwaka huu kuna uchaguzi wa serikali za mitaa na mwakani 2025 kuna Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, hivyo wananchi wanapaswa kutoa taarifa dhidi vitendo vinavyoashiria rushwa.
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kunakuwa na ustawi wa wananchi pia uwajibikaji kwa wananchi.
“Watanzania hawawezi kufanikiwa au kufikia lengo la ustawi iwapo jamii itaendelea kuendekeza vitendo vya rushwa,” amesema Mwaiswelo.
Amesema rushwa ikiendelea, lengo la kufikisha huduma kwa wananchi kama vile huduma za afya, elimu pasi kupambana na ruhwa haviwezi kuwafikia wananchi.
Amesema Serikali imekuwa ikikemea vitendo vya rushwa na kuwataka wananchi kuwa sehemu ya kudhibiti na kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa.
Ameeleza viongozi wengi wasiobora wanatokana na rushwa, hivyo wananchi wanapoendelea kuchagua viongozi wa aina hiyo ni kujichelewesha kupata maendeleo.
“Viongozi wa aina hiyo hawawezi kuwa na uchungu na maisha ya wananchi kwa sababu viongozi wa aina hiyo lengo leo ni kupata uongozi na siyokuwaletea wananchi maendeleo,” amesisitiza Mwaiswelo.
Amesema:“Viongozi ambao wanakuja kwa wananchi kwa lengo la kutoa kanga wanapaswa kukataliwa kwa namna yoyote kwa sababu hawafai kuwa viongozi.”
Amesema Watanzania wanafanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano hivyo wananchi wanapaswa kutouza kadi za mpigakura kwa sababu baada ya kuingia madarakani hawataweza kuwawajibisha hadi ifike kipindi kingine cha uchaguzi.
“Kuuza kadi za mpiga kura itawafanya kukosa viongozi bora. Hii nchi ni ya mfumo wa vyama vingi na hakuna nafasi ya wagombea binasi hivyo, kamati za siasa zichague wagombea ambao wataleta tija kwa taifa hili,” amesema Mwaiswelo.
Amesema vyama vya siasa vinapaswa kuwapitisha viongozi ambao wanajua lengo hasa la Serikali kwamba ni kuwaletea wananchi maendeleo.
Vijana wahamasishwa, watahadharishwa
Amewataka vijana kujihusisha na maendeleo ya nchi hii kwa kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa.
Pia, amewatala vijana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, huku pia wakiwa tayari kutoa taarifa za viashiria vya rushwa.
Amesema maendeleo ambayo Serikali ina lengo la kuyafikisha kwa wananchi hayawezi kufanikiwa kama tutakuwa na kizazi ambacho kinafumbia vitendo vya rushwa.
Amesema kina mama wamekuwa wepesi kujitokeza katika kupiga kura au kwenye kampeni, lakini wanatakiwa kujiepusha na wagombea ambao wanajihusisha na vitendo vya rushwa.
“Kuchaguza maendeleo au umasikini ni uamuzi wa wananchi wenyewe,” amesema Mwaiswelo.
Amesema amesema taasisi hiyo ipo mbioni kubandika vipeperushi vyenye ujumbe wa kudhibiti na kupambanana na rushwa katika ofisi mbalimbali za vyama vya siasa nchini kama ilivyofanya katika sekta ya afya ili kuongeza uelewa kwa wananchi wao.
Amefafanua kwamba wanannchi wanapaswa kuchagua maendeleo kwa kuchagua viongozi bora ili kuondokana na umasikini.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Sulum Hamduni akizungumza katika warsha ya wadau katika tasnia ya habari akisema rushwa ni chanzo za upatikanaji viongozi wasio na madili.
Alisema rushwa inadhoofisha utawala bora na demokrasia ambapo baadhi ya wananchi wenye sifa za uongozi bora kushindwa kugombea au kutoteuliwa au kuchaguliwa kwa kutokuwa tayari kutoa hongo.
“Rushwa inasababisha uvunjifu wa amani kutokana na migogoro ya mara kwa mara ya kisiasa na kusababisha Taifa kuendelea kugubikwa na rushwa,” alisema Hamduni.