Mkurugenzi Mtendaji NIC atoa wito kwa wawekezaji kukata Bima

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Bima (NIC), Kaimu Abdi, amewataka wawekezaji nchini kukata bima za biashara zao ili waweze kufidiwa pindi wanapopatwa na majanga.

Alitoa wito huo leo, Julai 9, 2024, jijini Dar es Salaam alipotembelea banda la NIC katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba.

Akizungumza katika maonesho hayo, Kaimu Abdi, amesema shirika la NIC limekuwa likitoa aina mbili za bima muhimu kwa ustawi wa nchi.

“NIC ni shirika la umma, hivyo tunatoa bima aina mbili: bima za maisha na zisizo za maisha. Bima hizi zinawagusa moja kwa moja wawekezaji kwani mwekezaji akipata majanga, tunaweza kumfidia na akaendelea na uwekezaji wake kama kawaida,” almesema Abdi.

Ameeleza kuwa bima zisizo za maisha zinahusiana moja kwa moja na kauli mbiu ya maonesho hayo isemayo “Tanzania: Mahali Salama pa Biashara na Uwekezaji.”

Pamoja na kuwa ni taasisi ya serikali, NIC pia inafanya biashara na inajukumu la kulipa kodi na kuwahudumia Watanzania.

Akizungumzia mikakati waliyojiwekea kwa mwaka huu wa fedha kuhusu kutoa uelewa kwa wananchi, Abdi alisema wamejipanga kuwafuata wananchi walipo na kuwapa elimu ya bima.

“Tulichogundua ni kwamba wananchi wengi hawana elimu ya bima. Sasa tumejipanga kuhakikisha tunawafuata huko huko walipo na kuwapa elimu hii. Bima ni muhimu na huwezi kuona umuhimu wake kama hayajakukuta majanga. Hatusubiri yakukute, tutahakikisha elimu inawafikia kila mmoja ili waweze kujiunga na bima,” aliongeza Abdi.

Related Posts