MIRATHI YA HANSPOPE: Baba, mtoto yaamriwa wakamatwe

MAHAKAMA Kuu iliyopo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia (IJC) Temeke, Dar es Salaam imetoa hati ya kukamatwa mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Z.H. Poppe Ltd, Caeser Hans Poppe na mwanaye Adam Caeser HansPoppe, kwa kuidharau.

Mahakama hiyo imeelekeza Caeser na Adam ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo wakamatwe na kupelekwa  mahakamani hapo Julai 19, 2024 ili washtakiwe kwa kosa la kuidharau mahakama.

Caeser ni mdogo wake Zacharia Hans Poppe ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, ametakiwa afike mahakamani hapo baada ya kukaidi amri ya mahakama hiyo kwa kushindwa kuitikia wito kwenye shauri la mirathi ya marehemu Hanspope

Hati hiyo ya kukamatwa wawili hao ambayo Mwananchi imefanikiwa kuiona, ilitolewa Julai 4, 2024 na Jaji Glady’s Nancy Barthy baada ya watu hao kushindwa kufika mahakamani tarehe hiyo iliyopangwa.

Caeser alitakiwa kufika kwa ajili ya kueleza hali ya mali za Zacharia HansPoppe ikiwemo taarifa ya mapato na matumizi, lakini hakutokea.

Jaji Barthy alifikia uamuzi huo baada ya watoto wa marehemu HansPoppe, Angel na Abel kuomba mahakama hiyo iamuru na imuite baba yao mdogo ambaye ni Adam Caeser atoe taarifa ya fedha ikiwemo mapato na matumizi yaliyopo katika kampuni ya baba yao mzazi iitwayo Z.H.Poppe ambayo kwa sasa inasimamiwa na Adam.

Katika maombi hayo Wakili Regina Herman anayemsimamia Analisa Zacharia Poppe, ambaye ni mtoto mkubwa wa marehemu Zacharia aliomba mahakama hiyo itoe adhabu kali dhidi ya wakurugenzi hao kwa kukaidi amri halali ya mahakama hiyo.

Wakili Herman alidai mteja wake alimuomba Caeser na Adam waitwe mahakamani hapo kwa sababu wao ndio walioshikilia hisa na mali za Zacharia katika kampuni zake na pia wanadaiwa kuendesha kampuni hiyo bila kuwashirikisha warithi ambao ni watoto.

Ombi la kukamatwa kwa wakurugenzi hao liliungwa mkono na wakili Emmanuel Msengezi anayewatetea wasimamizi wawili wa mirathi ya Zacharia, ambao ni Angel Zacharia Poppe na Abel Zacharia Poppe. Msengezi alidai katika kampuni hizo, Zacharia  anamiliki hisa kwa asilimia 90 wakati Caeser ana asilimia 10.

Msengezi alidai baada ya kuwasilisha maombi hayo waliomba mahakama itoe hati ya wito ili Adam aweze kufika mahakamani hapo kwa kwa kuwa mkurugenzi huyo anaendelea kushikilia mali za marehemu Zacharia, huku akiendelea kukopa kwa jina la kampuni na akishindwa kulipa madeni ya kampuni hizo.

Alidai kampuni za Zacharia inaingiza fedha nyingi, lakini halipi madeni huku warithi wa kampuni hiyo ambao ni Abel na Angel akikataa kuwaingiza katika kampuni ili wawe wasimamizi.

Chimbuko la hati ya kukamatwa linatokana na kesi ya mirathi marehemu Zacharia, namba 177 ya mwaka 2022 iliyofunguliwa katika mahakama hiyo.

Kesi hiyo ipo katika hatua ya usikilizwaji ambapo Julai 4, 2024 iliitwa kwa mahakama kusomewa orodha ya mali iliyokusanywa na kutoa taarifa ya kufungwa kwa hesabu na namna mali hizo zilivyogawanywa, lakini wakurugenzi hao hawakufika mahakamani na ndipo mawakili wa wasimamizi wa mirathi walipowasilisha ombi kwa mahakama kutoa hati ya kuwakamata.

Zacharia HansPoppe alifariki dunia Septemba 10, 2021 katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu na mazishi yake yalifanyika Septemba 15, 2021 mkoani Iringa.

Hans Poppe anakumbukwa na wanachama wa Simba na klabu hiyo kwa kuiletea mafanikio makubwa kutokana na uhamasishaji alioufanya baada ya kuteuliwa na pia kuwa mwenyekiti wa kundi la marafiki wa Simba ‘Friends of Simba’ ambalo lilijizolea umaarufu mkubwa katika medani za mchezo wa soka hapa nchini.

Related Posts