Dar es Salaam. Hatimaye wakili Boniface Mwabukusi aliyeenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), amepata marejeo ya uamuzi wa Kamati ya Rufaa na anatarajiwa kuyawasilisha mahakamani kesho Julai 10.
Mwabukusi aliyekuwa miongoni mwa wagombea sita wa nafasi hiyo, alitangaza kupinga uamuzi uliotolewa Julai 6, 2024 na kamati hiyo.
Wagombea wengine ni pamoja na Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Ibrahim Bendera, Sweetbert Nkuba na Paul Kaunda ambao sasa wameanza kampeni kwa ajili ya uchaguzi utakaofanyika Agosti 2, 2024 jijini Dodoma.
Akizungumza na Mwananchi, Julai 6, 2024 Katibu wa Kamati ya Rufaa, Nelson Frank alisema walimkuta na kosa la kimaadili Mwabukusi baada ya kusikiliza pingamizi alilowekewa, linalohusisha onyo alilopewa na Kamati ya Maadili ya Mawakili.
Hata hivyo, Mwabukusi amepinga uamuzi huo akisema hukumu ya Kamati ya Maadili ya Mawakili haina mashiko kwa kuwa hakukosea kuwakosoa viongozi wa Serikali kuhusu makubaliano ya uwekezaji wa bandari kati ya Serikali ya Dubai na ya Tanzania.
Pia, alisema hukumu aliyopewa ya onyo iliishia pale, kwa hiyo haimzuii kugombea uongozi ndani ya chama hicho na kwamba ameshakata rufaa.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 9, 2024 Mwabukusi amesema tayari ameshachukua uamuzi mahakamani leo watauingiza mahakamani kwa hati ya dharura.
“Tayari tumeshachukua marejeo ya uamuzi wa kamati ya rufaa na kesho tutawasilisha mahakamani kwa hati ya dharura, niwaondoe hofu wananchi haki yangu itapatokana kabla ya uchaguzi,” amesema.
Kuenguliwa kwa Mwabukusi kumeibua mjadala miongoni mwa mawakili, huku baadhi yao wakiahidi kuususia uchaguzi huo.
Miongoni mwao ni Wakili Michael Mwagasa aliyesema kuwa Mwabukusi ni wakili mwandamizi na sifa zote za kuwa mgombea urais wa TLS.
“Kikubwa ni kwamba apewe nafasi ya kusikilizwa na Kanuni ziweze kutafsiriwa sawasawa kama wale waliomuengua kwenye uchaguzi huo ni kweli wanayo hayo mamlaka kisheria? Kama hawana basi maamuzi yao ni batili na ni kama hayapo,” amesema.
Naye mgombea urais wa chama hicho, Emmanuel Muga amesema Mwabukusi hakuondolewa kihalali.
“Kwa kusoma kanuni zinazoratibu chaguzi za TLS, ni dhahiri sioni popote ambapo kamati ya rufaa ingemwengua Mwabukusi na hapakuwa na sababu zozote za kisheria za kumwengua.
“Naunga mkono hatua yake ya kwenda mahakamani ila siungi mkono hatua yake ya kuwataka mawakili kususia mkutano mkuu na uchaguzi,” amesema.
Ameongeza kuwa mawakili ni wanasheria hupambana na dhuluma kwa kutafuta ufumbuzi wa kisheria siyo kususia.
“Wakili Mwabukusi inabidi aachiwe agombee na ashinde au ashindwe kwa sera zake. Siyo hatua hii inayoweza kutafsiriwa kuwa wanamweka pembeni kwa kumwogopa,” amesema.
Mwenyekiti wa mawakili vijana wa TLS, Edward Heche alisema wigo wa ushindani haufai kuminywa katika chama hicho.
“Chama kinahitaji kiongozi ambaye ana maono anaweza kuyabeba kwanza maono ya chama cha sheria, maono ni hayo ni pamoja na chama kusimamia mambo mawili kwanza kabisa mambo ya wanachama na pili umma.
“TLS lazima itetee wanachama na maslahi yake na pia itetee umma kwa ujumla, ndiyo maana Boniphace Mwabukusi alikuwa anaonekana ni mtu mwenye sifa hizo,” alisema.