Maghorofa Dar yashuka bei, kiini chatajwa

Matokeo ya sensa ya majengo ya mwaka 2022 yanaonesha kuwa idadi ya majengo yote Tanzania ni 14,348,372 ambapo 13,907,951 yapo Tanzania Bara na majengo 440,421 yapo Tanzania Zanzibar.

Aidha majengo mengi (asilimia 94.4) Tanzania siyo ya ghorofa. Majengo tisa kati ya kumi ni kwa ajili ya makazi na asilimia 3.4 ni ya biashara – makazi. Kwa upande mwingine, asilimia 98.0 ya majengo yote ya makazi na biashara – makazi ni ya uniti moja.

Maeneo ya vijijini yana jumla ya majengo 10,038,201 na maeneo ya mijini yana jumla ya majengo 4,310,171 na idadi kubwa ya majengo kwa Tanzania Bara ipo katika Mkoa wa Dar es Salaam (913,707), ukifuatiwa na Mwanza (868,430) na Dodoma (836,909).

Ukitokea mkoani kuja Dar es Salaam miongoni mwa masuala ya kushangaa ni wingi wa majengo marefu na kwa mujibu wa sena jiji hilo lilikuwa na jumla ya maghorofa 32,219 hadi mwaka 2022.

Baadhi ya watu waliozoea nyumba za chini ni hali ya kawaida kutamani kuishi au hata kufanya kazi kwenye jengo la ghorofa na baadhi ya waishio nje ya mji hutamani kuishi mjini yalipo maghorofa.

Loading...

Loading…

Kama ilikuwa kiu yako kuwa na ofisi au makazi katika ghorofa na gharama kubwa ya kodi ya pango ndiyo iliyokuwa kikwazo, pengine huu ni wakati mzuri wa kutimiza ndoto yako.

Hiyo inatokana na kupungua kwa zaidi ya nusu ya bei ya pango katika majengo ya maghorofa kadhaa nchini, kwa mujibu wa ripoti ya uthabiti wa kifedha Tanzania ya mwaka 2023, iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Ripoti hiyo iliyohusisha majengo 13 ya biashara na makazi, inaonyesha kati ya hayo, saba bei ya pango lake ilishuka mwaka 2023, ikilinganishwa na mwaka 2022.

Lakini, hali ilikuwa tofauti kwa majengo matatu ya maghorofa, ambayo kwa mujibu wa ripoti hiyo, bei yake ya pango ilisalia bila kubadilika katika kipindi cha miaka hiyo na matatu mengine bei iliongezeka.

Kwa kipindi cha mwaka mmoja kutoka Desemba 2022 hadi Desemba 2023, unaonyesha mita moja ya mraba katika jengo la Golden Jubilee Desemba 2022 ilikuwa Sh36,000, lakini Desemba mwaka 2023 ilikuwa na kuwa Sh25,000.

Hali kama hiyo ilishuhudiwa katika jengo la Twin Towers (majengo pacha), ambalo kodi ya mita moja ya mraba iliyokuwa Sh32, 000 mwaka 2022 ilipungua hadi kufikia Sh25, 000.

“Jengo la The International House Property kodi ilipungua kutoka Sh28, 000 hadi Sh25, 000 kwa mita ya mraba katika kipindi cha mwaka huo mmoja,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Mafao House nalo, kodi yake imeshuka kutoka Sh16,000 hadi Sh12,000, kama ilivyo kwa Samora Avenue lililopungua bei ya kodi kutoka Sh18,000 hadi Sh16,000 na PSSSF Tower I ambayo mwaka 2023 mita ya mraba inapangishwa kwa Sh17,000 kutoka Sh18,000 ya mwaka 2022. Bei hizo ni kwa mita moja ya mraba.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, bei ilishuka hata katika jengo la Quality Plaza kutoka Sh22, 000 hadi Sh21, 000 kwa mita ya mraba.

Ingawa kupungua kwa kodi hizo ni fursa kwa wapangaji, kwa wamiliki ni maumivu, lakini maendeleo ya teknolojia yaliyosababisha kazi nyingi kufanywa mtandaoni inatajwa kuwa moja ya sababu, kama inavyoelezwa na Mwanazuoni wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora.

Mhadhiri huyo alisema maendeleo ya sayansi na teknolojia yanasababisha kazi nyingi kufanyika mtandaoni na hivyo wateja wa ofisi za kupanga wanapungua.

“Wakati mwingine wateja wa kupanga katika majengo hayo wanapungua kwa sababu wengi wanaanzisha kampuni mtandaoni na wanaweza kufanya huko bila kuwa na ofisi,” alisema Profesa Kamuzora.

Kuongezeka kwa majengo hayo ni sababu nyingine, inayotajwa na mwanazuoni huyo kama chachu ya wamiliki kushusha bei, akifafanua wanalenga kuvuta wateja.

“Tumewahi kufanya utafiti unaofanana na huo, bei kushuka hii inamaanisha majengo yamekuwa mengi (supply), kama ‘supply’ ni kubwa itabidi kuwe na msawazo wa biashara ambapo inalazimu wamiliki kupunguza bei ili wateja waongezeke,” alisema.

Janga la Uviko-19 nalo lililosababisha kampuni nyingi kufunga ofisi zake, kwa mtazamo wa Mack Patrick mtaalamu wa uchumi, ni sababu nyingine ya kupungua kwa kodi hiyo.

“Uviko-19 ulivyoathiri sekta ya utalii ni sawasawa na kwenye sekta ya milki, kwa sababu mzunguko wa biashara ulikuwa mdogo duniani kote na majengo hayo mara nyingi wapangaji wake ni sekta binafsi ambazo miaka mitatu nyuma ziliyumba.

“Wakati mwingine katika uchumi unapunguza bei ya bidhaa ili upate wateja wengi, ndio hicho kinachofanyika,” alisema.

Meneja wa Uwekezaji wa jengo la Johari Rotana Tanzania, Doris Zeng alionyesha mtazamo tofauti, akigusia mahali lilipo jengo husika na bei ya kupangisha ni sababu za kukosa wateja.

“Naamini ni mambo mawili, moja ni eneo, ikiwa wateja wako watarajiwa wako Masaki, utapata ofisi Masaki, na hautachukua ofisi katikati ya jiji. Sababu nyingine ni bajeti, baadhi ya kampuni ndogo haziwezi kumudu pango na gharama katika jengo,” alisema Doris.

Mengine bei haijabadilika

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kodi ya pango katika Jengo la Benjamini Mkapa ilisalia kuwa Sh20,000 kwa mita ya mraba, kadhalika jengo la Social Security House ikibaki kuwa Sh16,000 na hata Commercial Complex Sam Nujoma haikubadilika ilibaki kuwa Sh27,000.

Wakati bei za pango zikishuka katika majengo mengi, ripoti hiyo pia inaonyesha kwa miaka mitatu mfululizo wastani wa kiwango cha upangaji katika majengo kinazidi kuongezeka.

“Wastani wa kiwango cha upangaji katika majengo ya biashara mwaka 2020 kilikuwa asilimia 80, mwaka 2021 kiliongezeka hadi asilimia 81 na mwaka 2022 kilifika asilimia 85,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Kuhusu kuongezeka kwa idadi ya wapangaji katika majengo hayo, ripoti inasema kunasababishwa na mzunguko wa biashara kuongezeka baada ya athari za Uviko-19 kupungua.

“Sekta ya milki iliendelea kupata nafuu kutokana na janga la Uviko-19 huku kiwango cha umiliki wa mali za kibiashara kikiongezeka kwa wawekezaji wa sekta hiyo. Viwango vya umiliki kuongezeka vinahusishwa na uboreshaji wa mazingira ya biashara, miundombinu na mahitaji,” kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Wakati bei ikishuka na kusalia kama ilivyokuwa kwa baadhi ya majengo, mengine yamepandisha bei likiwemo Rita Tower kutoka Sh16, 000 hadi Sh20, 000 kwa mita ya mraba, kama ilivyoelezwa na ripoti hiyo.

Victoria House nalo lilipandisha bei kutoka Sh16,000 ya mwaka 2022 hadi Sh18,000, huku PSSSF Tower II ikiongeza kutoka Sh23,000 hadi Sh25,000 kwa mita ya mraba.

Hata hivyo, ripoti hiyo imetaja sababu za kuongezeka kwa bei katika majengo hayo ni; “Ongezeko la mapato ya kaya kadri hali ya uchumi inavyoimarika na msukumo wa mahitaji kutokana na ukuaji wa idadi ya watu na ukuaji wa miji.”

Kwa mtazamo wa kiuchumi, kupungua kwa kodi katika majengo hayo kunasababishwa na ugumu wa maisha unaowafanya wananchi kuhama katikati ya Miji na kukimbilia pembezoni kama anavyoeleza Dk Abel Kinyondo mtaalamu wa uchumi.

“Watu wengi waliokuwa wanakaa karibu na mijini kwa sasa wanajaribu kurudi nyuma, ukiangalia sasa hivi hata kampuni nyingi zimechukua ofisi Morocco, tofauti na zamani zilikuwa zinagombea Posta,” anasema.

Kama kampuni zinakimbilia Morocco, anasema wananchi watakimbia mbali zaidi na hasa pembezoni mwa miji.

Dk Kinyondo anasema sababu nyingine, anasema ni wingi wa majengo ilhali wahitaji ni wachache, hivyo ili kukamata soko wamiliki hawana budi kushusha bei. “Watu wanaohitaji wanakuwa wachache”

Alichokisema Dk Kinyondo hakitofautiani na kile ambacho Mwananchi ilikishuhudia pembezoni mwa barabara ya Bagamoyo jijini Dar es Salaam ambayo unaweza kuiita Silicon Valley ya Tanzania .

Kampuni kubwa za na za kati hapa nchini zinapendelea kuweka makao yake makuu au ofisi zake katika barabara hiyo kuanzia Morocco hadi Mwenge na nyingine maeneo ya Mbezi Beach na Tegeta.

Pamoja na kuwa bei kodi ya pango kwa wastani unaonyesha kupungua katika majengo mengi hapa jijini lakini kwa kipande cha kutoka Morocco hadi Mwenge pengine bei imeongezeka kwani ni kubwa kuliko majengo mengi ya mjini.

Katika majengo kama Tan House, Victoria Palace, Tanzanite Park, Noble House na Mwanga Towers upangishaji wa ofisini ni kati ya Dola za marekani 10 (Sh26,000) hadi 14 (Sh37,000).

Zaidi kuhusu biashara ya majengo

Ripoti ya ‘Muhtasari wa Pato la Taifa Robo ya Pili ya mwaka 2023’ iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaonyesha shughuli za upangishaji majengo ilikua kwa asilimia 4.2 huku kinara wa ukuaji ikiwa ni shughuli ya kiuchumi ya fedha na bima iliongoza kwa asilimia 15.6.

Wakati ukuaji wa shughuli hiyo ukiwa wa Wastani, Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inasema Tanzania ina jumla ya majengo milioni 14.3 ambapo kati yake ya ghorofa ni 68,724 sawa na asilimia 0.47.

Kwa mujibu wa tovuti ya Statista thamani ya sekta ya milki duniani ni Dola za Marekani trilioni 637.8 hadi mwaka 2024.

Aidha, takwimu hizo zinasema sekta hiyo inatarajia kukua kwa asilimia 3.41 na thamani yake inatarajiwa kuwa Dola za Kimarekani trilioni 729.4 ifikapo mwaka 2028.

Nchi ya China inaongoza kuwa na thamani kubwa katika sekta ya milki duniani ikikadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani trilioni 135.7 hadi mwaka 2024.

Related Posts