Trafiki waliodaiwa kuchezea mashine wafutwa kazi

Moshi. Jeshi la Polisi nchini Tanzania limewafukuza kazi na kuwafuta jeshini askari wake wanne wa usalama barabarani Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kufuta picha kwenye kamera za jeshi hilo walizokuwa wanatumia kupima mwendokasi wa madereva.

Taarifa ya Msemaji wa Jeshi hilo, David Misime aliyoitoa leo Jumanne, Julai 9, 2024 imesema askari hao walifukuzwa kazi jana Jumatatu baada ya kushtakiwa kijeshi na kupatikana na hatia.

“Mtakumbuka Mei 30, 2024 Jeshi la polisi lilitoa taarifa ya kushikiliwa askari polisi wanne kwa ajili ya uchunguzi, askari hao walikuwa wanafanya kazi Kitengo cha Usalama Barabarani Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro,” amesema Misime.

“Baada ya uchunguzi kukamilika ilibainika askari hao walikuwa wamefuta picha kutoka kwenye kamera za Jeshi la Polisi walizokuwa wanatumia kupima mwendo kasi (speed rader) wa madereva waliokuwa wamekiuka Sheria za Usalama Barabarani kwa maslahi yao binafsi.”

Aidha amesema askari hao walishtakiwa kijeshi na wakapatikana na hatia na hivyo Julai 8, 2024 walifukuzwa kazi na kufutwa jeshini.

Mei 2024, Mwananchi walikuwa wa kwanza kuripoti taarifa za wizi wa fedha za umma kupitia mifumo ndani ya jeshi hilo katika mikoa ya Iringa, Pwani na Kilimanjaro wanadaiwa kuingia matatani.

Chanzo chetu kilidokeza trafiki hao kwa miaka miwili, inadaiwa walikuwa wakipiga picha magari yanayovunja sheria kwa kwenda mwendo kasi eneo lisiloruhusiwa, kisha kufanya mazungumzo na madereva na kuchukua fedha.

 Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi

Related Posts