Dar es Salaam. Treni ya Umeme ya Kisasa (SGR) imeonekana kuwavutia wasafiri wengi tangu ilipoanza kutumika nchini, ikisafirisha abiria zaidi ya abiria 4,000 kwa siku, kwa mujibu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC).
Idadi ya abiria wanaosafiri kwa treni hiyo kwa siku imefikia kiwango hicho katika kipindi ambacho safari pekee zinazofanyika ni katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro.
Kwa mujibu wa TRC, idadi ya abiria wanaosafiri kwa SGR kwa siku inatarajiwa kuongezeka mara mbili ya wanaotumia sasa, pindi zitakapozinduliwa safari za Dodoma mwishoni mwa mwezi huu.
Kwa kawaida ingechukua zaidi ya mabasi 70 kusafirisha abiria 4,000, jambo linaloonyesha dalili ya mapinduzi katika sekta ya usafirishaji hasa utakapoanza ule wa mizigo.
“Matokeo yamekuwa makubwa sana. Tunavyoongea, tiketi zote za treni ya saa 10:00 jioni leo (Jumatatu, Julai 8, 2024), zimeuzwa na pengine hata ile ya kesho asubuhi (leo Jumanne Julai 9, 2024) nayo imeuzwa,” amesema Masanja Kadogosa, Mkurugenzi wa TRC.
Treni hizo zilianza kutoa huduma ya usafiri kwa njia ya Dar es Salaam hadi Morogoro Juni 14, 2024, huku safari za Dar es Salaam kwenda Dodoma zikitarajiwa kuanza Julai 25.
Kwa mujibu wa Kadogosa, zitakapoanza safari za Dar es Salaam kwenda Dodoma, kutafanyika mabadiliko ya muda, akidokeza pengine treni itaanza safari kutoka Dar es Salaam saa 11:00 alfajiri badala ya saa 12:00 asubuhi.
Sambamba na hilo, amesema shirika hilo litaanzisha treni itakayoondoka Dar es Salaam saa 2:30 asubuhi.
“Mtu anayekwenda kutembea lazima achague treni ya saa 2:30 asubuhi, ili kutoa nafasi kwa abiria wanaosafiri kwa shughuli za kibiashara na za dharura kama vile mikutano, watapanda ya saa 11:00 alfajiri,” amesema.
Kadogosa amesema pia wameanzisha maegesho ya magari katika kituo cha Dar es Salaam yatakayoegesha magari 500 kwa wakati mmoja.
“Lengo ni kuwezesha teksi na ndugu wanaowasubiri abiria kuegesha magari yao wakati wakisubiri kuwasili kwa treni,” amesema.
Hata hivyo, ameeleza kituo cha Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) kilichopo nyuma ya kituo cha SGR cha Tanzanite, karibu na Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, pia kitasaidia kufikisha abiria eneo hilo.
“Ili kuepuka msongamano, kabla ya treni kuwasili katika Kituo cha Dar es Salaam, wanapaswa kuanza kuomba teksi treni inapokaribia kufika,” amesema.
Akielezea tofauti kati ya treni hizo na zile za kawaida, Kadogosa amesema zote ni za SGR, lakini za kisasa zinakwenda moja kwa moja hadi Morogoro bila kusimama kituo chochote, wakati ya kawaida ina vituo kadhaa vya kusimama.
Amesema mkazi wa Pugu anaweza kusubiri treni ya haraka ikiwa atakwenda kupanda katika kituo cha Dar es Salaam (kituo cha Tanzanite) na kinyume chake.
Amesema treni ya kawaida inasimama katika vituo vinne kabla ya kufika Morogoro ambavyo ni Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere na mwisho Morogoro.
“Abiria anaweza kuomba tiketi ya kupanda treni katika kituo chochote kati ya vituo vilivyotajwa tofauti na treni za haraka ambapo abiria anaweza kupanda tu katika kituo cha mwanzo,” amesema.
Mtu analipa Sh20,000 kwa tiketi ya daraja la kawaida kusafiri kwa treni ya haraka kati ya Dar es Salaam na Morogoro, wakati abiria wa daraja la biashara na kifalme wanalipa Sh35,000 na Sh45,000 mtawalia.
Kwa treni ya kawaida, tiketi ya Dar es Salaam-Morogoro inagharimu Sh13,000 na Sh21,000 kwa daraja la kawaida na biashara mtawalia.
Kwa upande wa muda, treni ya haraka inaokoa kati ya dakika 20 hadi 30 katika safari ya Dar es Salaam-Morogoro na kwamba safari ya Dar es Salaam-Dodoma itakapoanza, muda halisi unaookolewa unaweza kuwa hadi saa moja.
“Unaposafiri kwa treni ya haraka kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ndipo unaweza kuona tofauti na kuchagua ni treni gani ya kupanda,” amesema.
Amebainisha treni ya haraka ni kwa abiria wenye shughuli za dharura kama biashara, kazi, mikutano na masuala mengine yanayohusiana na hayo.
“Treni ya haraka ikianza saa 11:00 alfajiri inafika saa 12:30, ikimaanisha kwamba mtu anayeishi Morogoro anaweza kufanya shughuli zake za kila siku akiwa Dar es Salaam,” amesema.