Lushoto. Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani amewataka majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuhakikisha wanashughulikia mashauri mapema na kuondoa mianya yote inayochelewesha mashauri hayo, ili haki ipatikane kwa wakati.
Siyani amenena hayo wakati akifungua mafunzo elekezi ya majaji wanne wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania jana Julai 8, 2024 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) mkoani Tanga.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na IJA na yanalenga kuwaandaa na kuwapatia ujuzi na maarifa muhimu Majaji hao, yatakayowaongoza katika utendaji wao wa kazi hiyo ya Mahakama Kuu.
“Majaji wa sasa ni lazima mjenge utamaduni wa kusoma nyaraka zote muhimu na kuwa tayari kujifunza kutoka kwa wenzetu walioondokana na tatizo la ucheleweshaji, mnapaswa kuhakikisha kila hatua ya shauri inapangiwa muda stahiki wa kukamilika.
“Nafahamu zipo sheria zinazotoa mwanya wa ucheleweshwaji, itakuwa ni jukumu lenu kuhakikisha mnaziba huo mwanya ili haki ipatikane kwa wakati,” amesema Jaji Kiongozi.
Pia Jaji Siyani ameongeza kuwa, malengo ya Mahakama ya utoaji haki yatafikiwa endapo kila ofisa ndani ya Mahakama atatimiza vema majukumu yake.
“Malengo ya Mahakama ya utoaji haki yatafikiwa endapo kila jaji, msajili, hakimu au msaidizi wa sheria atasimamia mambo yote muhimu tangu shauri linafunguliwa mahakamani mpaka linahitimishwa,” amesema na kuongeza:
“Msiamini kuwa mnajua kila kitu, kazi yetu ni ya kijifunza kila wakati, kusoma na kujifunza, na Jaji ambaye anataka kufanikiwa ni lazima ajifunze, ni lazima asikilize, ni lazima aongoze mahakamani.”
Awali akitoa neno la utangulizi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Revocate Mteule amewapongeza Majaji hao kwa kuteuliwa na kuwaomba kwenda kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuzitendea haki nafasi zao hizo walizokabidhiwa na umma.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha, Sylvester Kainda amesema kuwa ni jukumu lao wao kama majaji wapya kulinda viapo vyao kwa kufanya kazi kwa uaminifu na bila upendeleo.
“Ni wananchi kuendelea kuwa na imani na chombo hiki cha Mahakama na sisi ambao tumo ndani ya Mahakama ni jukumu letu kulinda viapo vyetu, kutenda kazi hizi ambazo tumekasimiwa na wananchi kwa uaminifu, bila upendeleo kama viapo vinavyosema na kila mtu apate haki yake kwa kadri sheria inavyoelekeza,” amesema Mhe. Kainda.
Majaji watatu kati ya wanne wanaopatiwa mafunzo hayo waliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Juni 6, 2024 na kuwaapisha Juni 13, 2024 katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, huku mmoja akiwa ameteuliwa Aprili 3, 2024.
Majaji hao ni pamoja na Sylvester Kainda, Projestus Kahyoza, Nehemia Mandia na Mariam Omary.
Aidha, mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya mafunzo ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2013, Mpango mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja na Mpango Mkakati wa Chuo cha IJA wa mwaka 2023/24-2027/28.