Rais wa Marekani Joe Biden amewakaribisha viongozi wakuu wa mataifa wanachama wa NATO mjini Washington kwenye mkutano huo wa kilele unaojikita katika kuipatia msaada zaidi Ukraine, lakini ambao pia unafuatiliwa kwa karibu na washirika wake nyumbani na nje, kwa uthibitisho kwamba rais huyo anaekabiliwa na shinikizo anaweza kuongoza bado.
Biden atetea mafanikio ya sera ya kigeni ya urais wake
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Biden ametetea mafanikio ya sera ya kigeni ya urais wake, na kusema hivi sasa jumuiya ya NATO imekuwa imara zaidi kuliko wakati wowote ule.
Soma pia:Viongozi wa NATO wakutana Washington chini ya wingu la vita
Hotuba ya Biden ilitanguliwa na picha za uingiliaji wa kihistoria wa NATO, kauli za marais wa Marekani kwa washirika na nukuu mbalimbali kuhusu maana ya “rafiki mzuri.”
Nchi za NATO kuipatia Ukraine mifumo ya ziada ya ulinzi wa anga
Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi wa mataifa ya NATO wameahidi kuipatia Ukraine mifumo mitano ya ziada ya ulinzi wa anga, zikiwemo betri za makombora ya Patriot na vifaa vingine vya mifumo ya Patriot.
Wameongeza kuwa katika miezi michache ijayo, wanakusudia kuipatia Ukraine dezani kadhaa za mifumo ya kimkakati ya ulinzi wa anga, mnamo wakati Urusi ikizidisha mashambulizi yake dhidi ya taifa hilo.
Baadhi ya nchi zatangaza msaada wao kwa Ukraine
Ujerumani na Romania zilikuwa tayari zimetangaza kwamba zitatuma mifumo yao miwili ya ulinzi na Uholanzi ilisema ilikuwa inashughulikia msaada kwa Kyiv, huku Italia pia ikitoa mfumo tofauti wa ulinzi.
Uongozi wa Biden watiliwa mashaka
Lakini maswali kuhusu uwezo wa Biden kuendelea kutawala yalitishia kuugubika mkutano huo huku rais huyo mwenye umri wa miaka 81 akikabiliwa na wito wa kujiengua kwenyekinyang’anyirocha muhula wa pili baada ya utendaji mbaya katika mdahalo dhidi ya mpinzani wake Donald Trump.
Biden asifu mataifa ya NATO kwa kujitolea katika ulinzi
Rais Biden pia ameyasifu mataifa ya NATO kwa hatua kubwa kuelekea kutimiza malengo ya kutenga asilimia 2 ya pato jumla ya ndani kwa ajili matumizi ya kijeshi, akisema wakati alipoingia madarakani mwaka 2020, ni mataifa tisa tu yaliokuwa yanatenga kiwango hicho, na mwaka huu idadi hiyo itafikia mataifa 23.
Soma pia:Shinikizo la kumtaka Biden kutowania muhula wa pili laongezeka
Katika mkutano huo unaoadhimisha miaka 75 ya kuasisiwa kwa jumuiya ya NATO, Rais Biden pia amemtunukuu Katibu Mkuu anaemaliza muda wake Jens Stoltenberg, Nishani ya Uhuru ya Rais wa Marekani, kwa kuuongoza muungano huo katika mmoja ya nyakati ngumu zaidi katika historia yake. Nishani ya Uhuru ndiyo heshima ya juu kabisaa ya raia nchini Marekani.
Biden asifu tabia ya utulivu ya Stoltenberg
Biden alisifu “tabia ya utulivu” ya Stoltenberg na kumuelezea kama “mtu mwadilifu, mwenye nidhamu” na “mwanadiplomasia aliekamilika.” Stoltenberg ameuongoza muungano huo tangu 2014, na atarithiwa katika nafasi hiyo mwezi Oktoba na waziri mkuu wa zamani wa Uholanzi Mark Rutte.
Mkutano wa NATO unaohudhuriwa pia na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, unafuatiliwa kwa karibu na Urusi, ambayo imesema inaichukulia jumuiya hiyo ya kijeshi kuwa inashiriki moja kwa moja katika mzozo wa nchini Ukraine.