Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda Julai 09, 2024 amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya King’s Trust International (KTI) Kusini mwa Jangwa la Sahara Bw. Andre Harriman kujadili namna ya kuwezesha ujuzi kwa Vijana ili wajiajiri na kuajiriwa.
Katika majadiliano hayo Prof. Mkenda amesema kutokana na maendeleo na mabadiliko ya teknolojia, juhudi za makusudi zinapaswa kuzingatiwa wakati huu, ambao unawategemea Vijana kushiriki kikamilifu katika sekta mbalimbali za uzalishaji ikiwemo viwanda.
“Nimewaambia sisi tunataka kupitia Vyuo vya VETA tushirikiane nao kuimarisha ujuzi maeneo mawili, moja kuchagua Vyuo viwili kuimarisha Vijana eneo la mekatroniksi, tuwafundishe namna ya kuwa fundi mahiri wa magari hasa yanayotumia vifaa vya kisasa” alisema Mkenda.
Aidha eneo la pili lililojadiliwa ni ufundi wa kushona nguo, Waziri huyo amesema kuna fursa nyingi kwa Vijana wa Kitanzania wanaweza kuzipata iwapo watangewa umahiri wa kutosha na kufundishwa Teknolojia mbalimbali, na hivyo kuwasaidia kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya KTI Bw. Harriman ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa namna inavyowekeza miundombinu ya Elimu, kuhakikisha Vijana wanapata elimu bora, na hivyo kupata wahitimu mahiri.
Amesema Taasisi hiyo ipo tayari kutembelea baadhi ya Vyuo vya VETA kujifunza zaidi na kuona namna ya kushirikiana Serikali kutimiza azma ya kuimarisha ujuzi kwa Vijana.
Cc:W/Elimu Sayansi na Teknolojia