Simulizi waumini wanavyolizwa pesa kanisani-1

Dar es Salaam. Kama ilivyo katika mataifa mbalimbali Afrika, nchini Tanzania, aina mpya ya viongozi wa dini inajitokeza, ikitumia mtaji wa watu maskini kujikusanyia mali.

‘Manabii’ hawa wa kisasa wameigeuza imani kuwa biashara yenye faida kubwa, wakitumia udhaifu wa wafuasi wao kujipatia mamilioni ya fedha.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini licha ya ‘manabii’ na ‘mitume’ hawa kuwa wanalitaja jina la ‘Yesu Kristo’ katika mahubiri yao, lakini namna madhabahu ya makanisa yao yanavyozalisha mamilioni ni jambo la kutupiwa jicho.

Katika jiji ambalo umaskini umekithiri na wakazi wake wanatafuta sana kazi, waume kwa wake wa kuoa na pia fedha za kumaliza kiu yao ya mahitaji mbalimbali, ‘mitume’ hao wanaahidi ustawi wao (wa kazi) kupitia utoaji, wakiwahimiza waumini wao kuacha fedha zao walizozipata kwa shida kwa kubadilishana baraka.

Matukio ya ‘makanisa’ hayo yanayochipuka yamekuwa yakiibua wasiwasi miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya kijamii na wachumi, ambao wanaona mwelekeo wa kutatanisha wa urundikaji wa mali unaofanywa na viongozi wa kidini kupitia mgongo wa wafuasi wao.

Mwandishi wa habari hizi akiwa katika ibada maalumu ya upako (wakati wa uchunguzi wake), alishuhudia wanawake wakileta bidhaa mbalimbali kutoka kwenye maduka na vibanda vyao ili kutoa sadaka kwa ‘manabii Mungu’ kwa matumaini ya kupata mtaji mkubwa.

“Hii ni sehemu ya mtaji wangu ambao tuliagizwa tuulete madhabahuni ili kupata zaidi,” anasema mwanamke mmoja na kudokeza: “Sijamwambia mume wangu kwa sababu asingeruhusu.”

Hivi ndivyo waumini hawa wameaminishwa, na kuwafanya kuuza mali zao ili kupata baraka zinazotarajiwa.

“Jirani yangu aliuza eneo lake la ardhi, akaleta pesa madhabahuni, na sasa amefanikiwa zaidi,” anasisitiza.

Chanzo kimoja ambacho hakikutaka jina lake liandikwe, ambacho huwaonyesha waumini sehemu za kukaa kanisani, kimefichua jinsi wachungaji maarufu wanavyofanya kazi kwa kupiga fedha.

“Katika ibada moja au kampeni moja ya kiroho, zaidi ya watu 50,000 huhudhuria. Kila muumuni mmoja anatakiwa kununua maji ya upako kwa Sh10,000, mafuta ya zeituni Sh20,000, chumvi Sh10,000 na yule anayehitaji kukutana na ‘mtumishi wa Mungu’ akiwa peke yake anatakiwa kupanga siku na angalau awe na Sh100, 000 ya kutoa.

“Pesa zinazokusanywa ni nyingi sana, na ni mwenye kanisa pekee ndiye anayejua la kufanya nazo,” kinasema chanzo hicho.

Chanzo hicho kinabainisha zaidi kuna upako maalumu ambapo muumini hulazimika kununua kitambaa cha upako kwa Sh30, 000 hadi Sh60, 000 licha ya mambo mengine ambayo nabii hujisikia kuyafanya ‘anavyoelekezwa na mungu.’

Muumini mwingine anahadithia kama hivyo, akisema: “Niliaminishwa bila baraka za ‘mtu wa mungu’,” sitafanikiwa kamwe. Niliishia kutumia akiba yangu yote kununua leso, keki, na chumvi zilizotiwa mafuta ya upako, kila moja ikidaiwa itaniletea mafanikio.”

Vitu hivyo, vinavyojulikana kama zana za miujiza, huuzwa kwa bei ya juu kuhakikisha mapato mazuri kwa watumishi hao wa mungu.

Uuzaji wa vitu hivyo vya ‘upako’ haufanyiki Tanzania pekee. Una mizizi pia katika nchi zingine, ukidhihirisha ni jinsi gani mtandao huo ulivyo mpana.

“Kuanzia siku ya kwanza niliguswa na mhubiri huyo, sielewi kilichotokea kwa sababu siku zote nilitaka kwenda na kuguswa tena na tena. Chochote alichokitaka kutoka kwangu, ningempa bila kufikiria mara mbili,” anaeleza muumini mmoja wa zamani ambaye alipoteza imani baada ya kuona hapati faida yoyote.

“Imani yangu iliposhuka, niliacha kwenda na hatimaye kurudi kusali kwenye kanisa langu la utotoni,” anasema.

Mitizamo ya wanasaikolojia

Wanasaikolojia wanaeleza viongozi hao wa dini hutumia udhaifu wa kisaikolojia wa wafuasi wao.

Dk Mwanaidi Chenge, mwanasaikolojia wa kimatibabu, anabainisha: “Kukata tamaa huzaa uzembe…wakati watu wanapotatizika kutafuta riziki, kuna uwezekano mkubwa wa kuamini miujiza na kutafuta ufumbuzi wa haraka. Manabii hao hutoa suluhisho linaloonekana kufanikisha matatizo yao, na kuwafanya kuwa shabaha rahisi.”

Udanganyifu wa kisaikolojia unazidishwa na ahadi za mafanikio, ambayo mara chache hutokea. Badala ya kuwahubiria waumini wao jinsi ya kuelewa maandiko matakatifu na kufanya kazi ili kuboresha maisha yao kupitia mbinu endelevu, wahubiri hawa wenye maneno mazuri uwahubiria injili ya utoaji.

Hili jambo si tu kwamba linaendeleza umaskini, bali pia linachepusha fedha kwa mahitaji ya msingi kwenye mifuko ya hawa ‘wanaojifanya’ watumishi wa Mungu. 

Uchunguzi huo umebaini kanisa moja la aina hiyo lilikusanya zaidi ya Sh10 milioni katika ibada moja kupitia uuzaji wa vitu vilivyotiwa upako. Kiongozi wa kanisa hilo, ambaye anaendesha magari ya kifahari na kuishi katika jumba la kifahari, anahalalisha utajiri huu kama malipo kutoka kwa Mungu kwa imani yake na uongozi wake.

“Nyie watu badala ya kumtolea maisha yenu Mungu, mnaendelea kufuata yale ambayo wengine hufanya. Nimeitwa na Mungu na ninawajibika kwake tu. Unafikiri tunaishi kwa sababu ya watu, hapana, ni kwa sababu ya Mungu,” ameliambia gazeti la Mwananchi alipotafutwa.

Chanzo kingine cha ndani ambacho (jina linahifadhiwa), kilifichua:”Kanisa hilo linamiliki biashara kadhaa, zote zikiwa zimesajiliwa chini ya jina la mtu huyo wa Mungu. Hii huhakikisha utajiri unabaki ndani ya udhibiti wake, na halipi kodi kutokana na hadhi ya kanisa hilo.

“Kukutana naye ana kwa ana ni mchakato mrefu; lazima ujulikane – wewe ni nani, unafanya nini, unaishi wapi, shida yako ni nini, kama umeolewa na hata majina ya watu wako wa karibu,” kinaeleza chanzo hicho.

Chanzo hicho kinasema kwa kujua mambo haya, itakuwa rahisi kwa mtume kuwaambia waumini wote kuhusu wewe wakati wa ibada ili kuonyesha kwamba alikujua kupitia ‘Roho Mtakatifu.’

Msamaha wa kodi unaotolewa na Serikali ya Tanzania kwa taasisi za kidini kumewezesha, bila kuelewa unyonyaji huo unavyofanyika. Hii ni kwa mujibu wa  wataalamu.

Wakati dini kuu hufuata vitabu vyake vitakatifu na kuzingatia ukuaji wa kiroho, madhehebu haya ya kileo (kisasa) yanatanguliza utajiri wa mali, mara nyingi kwa gharama za wafuasi wao.

Mwanatheolojia na mwanasosholojia maarufu, Yusuph Mkondya, anasema ukosefu wa ajira na uvivu umesababisha watu wengi kuanzisha makanisa yanayofadhiliwa na watu wenye nia mbaya.

“Tunawaona hata watu maarufu, kama wasanii na waigizaji wa vichekesho, wanakuwa wachungaji. Kwa baadhi ni njia ya kutumia ufasaha wao kujilimbikizia pesa kutoka kwa waumini wao, wengine hutumia kanisa kuficha shughuli zao zingine zisizojulikana katika jamii,” anasema.

Anaeleza katika baadhi ya nchi, wahubiri hao wamenaswa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya na biashara haramu ya binadamu.

“Kwa hiyo, usajili pekee haupaswi kuwa mwisho wa ufuatiliaji makini wa mamlaka,” anasema. 

Hali hii si ya Tanzania pekee. Matukio kama hayo yameripotiwa nchini Nigeria, Afrika Kusini, Kenya, Zimbabwe na hata katika nchi za Magharibi.

Hawa wachungaji, manabii, mitume wanatumia mbinu zilezile za kuuza vitu vya upako na kuahidi mafanikio.

Kadiri kutaniko linavyokuwa kubwa, ndivyo mapato yanavyoongezeka, na hivyo kutengeneza muungano wenye nguvu ambao ni vigumu kuuvunja. Nchini Afrika Kusini, nabii mmoja hivi karibuni alifichuliwa kwa kuuza mbegu za ‘miujiza’, na kuahidi kwamba zingekuwa miti inayozaa pesa.

Maelfu ya wafuasi waliokata tamaa walinunua na kujikuta wakiwa maskini zaidi na kukatishwa tamaa.

Chanzo kimoja kilifichua kuwa kililazimishwa kutoa ushuhuda wa uongo na baadhi ya manabii na mitume maarufu katika ukanda wa Afrika Mashariki, ili kuwashawishi watu kufuata huduma zao.

Udanganyifu kama huo umefichuliwa katika uchunguzi kama vile ripoti ya “Jicho Pevu” nchini Kenya, ambayo ilifichua wachungaji bandia wanaojihusisha na vitendo vya udanganyifu.

Kwa ujumla makanisa hayo kunachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la umaskini katika jamii, kwani fedha ambazo zingeweza kutumika kwa maendeleo huingizwa kwenye mifuko ya viongozi hao wa dini.

Usikose sehemu ya pili ya habari hii kesho 

Related Posts