Kagame kuendelea leo Dar | Mwanaspoti

BAADA ya jana kupigwa michezo minne ya ufunguzi wa michuano ya Kombe la Kagame, itaendelea leo na itakuwa ni zamu ya timu za kundi ‘B’, mechi zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa mapema utakuwa kati ya Al Hilal ya Sudan itakayocheza dhidi ya Djibouti Telecom ya Djibouti saa 12:00 jioni huku mabingwa mara tatu wa michuano hiyo, Gor Mahia ya Kenya itacheza na Red Arrows ya Zambia kuanzia saa 3:00 za usiku.

Michuano hiyo iliyoanza jana ikitarajiwa kuhitimishwa Julai 21, inawakilishwa na timu 12 kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati maarufu (Cecafa), zikiwa katika makundi tofauti na kundi ‘A’ ni Coastal Union (Tanzania), Al Wadi (Sudan), JKU (Zanzibar) na Dekedaha kutokea Somalia.

Al-Hilal Omdurman ya Sudan, Gor Mahia (Kenya), Red Arrows (Zambia) na Djibouti Telecom ya Djibouti zinaunda Kundi ‘B’ huku Kundi ‘C’ likiwa na timu za SC Villa (Uganda), APR (Rwanda), Singida Black Stars (Tanzania) na Al-Merrikh ya Sudan.

Meneja wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto alisema michuano ya msimu huu itasaidia timu ambazo zinashiriki kujipanga vizuri kwa ajili ya msimu ujao.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alisema, licha ya timu hiyo kupangiwa kundi gumu la ‘C’, lakini wamedhamiria kutwaa taji hilo.

Related Posts