KMC imeulizia uwezekano wa kupata saini ya kiungo Mkongomani anayeichezea Inter Club de Brazzavvile, Inno Jospin Loemba.
Klabu hiyo inamtazama Loemba kama mbadala wa Awesu Awesu ambaye amemaliza mkataba na timu hiyo akihusishwa na vigogo nchini Simba na Yanga.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Congo Brazzaville nje na KMC ana ofa pia kutoka Pamba Jiji.
COASTAL Union ipo kwenye hatua za mwisho kukamilisha dili la beki wa kushoto wa Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship, Antony Mligo.
Mbali na Coastal iliyomaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu uliopita, Namungo nao ilionyesha nia ya kutaka saini ya beki huyo.
Coastal imefuzu kucheza michuano ya kimataifa na inapambana kusuka kikosi chake mapema kwa ajili ya Kombe la Shirikisho Afrika.
KAGERA Sugar inakumbana na upinzani mkali kutoka kwa Singida Black Stars (Ihefu) kuwania saini ya mshambuliaji wa Rivers United, Nyima Nwanga.
Nwanga mwenye miaka 31 pia anaweza kuendelea kusalia Nigeria kutokana na mabosi wake wapo pia kwenye mazungumzo na klabu hiyo. Singida inataka kutengeneza kikosi imara na cha ushindani kuwania nafasi za juu kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao.
KAMA mambo yatakwenda sawa basi kiungo wa Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja msimu uliopita, Said Mkopi anaweza kujiunga na Mashujaa ya mkoani Kigoma.
Mazungumzo baina ya mchezaji na klabu hiyo bado yanaendelea na mpaka sasa yanakwenda vizuri na kuna uwezekano mkubwa wa kinda huyo kujiunga na Mashujaa.
Namungo imeanza kurekebisha kikosi hicho na tayari imefikia hatua nzuri na Kipa wa zamani wa Tanzania Prisons, Yona Amos. Kama Yona ataingia mkataba na Namungo atakutana na Beno Kakolanya anayehusishwa na wauaji hao wa Kusini.
Awali kipa huyo alikuwa akihusishwa na Yanga lakini dili hilo lilikufa baada ya kumpata Khomeiny Abubakar kutoka Ihefu.
FOUNTAIN Gate Princess inafuatilia uwezekano wa kupata saini ya kiungo mshambuliaji wa Yanga Princess, Zayonce Kalabani anayecheza kwa mkopo Amani Queens. Kiungo huyo amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na Yanga, hivyo Fountain iko tayari kuuvunja ili kupata huduma ya mchezaji huyo ambaye alionyesha kiwango kizuri akiwa na Amani.
KUNA uwezekano mkubwa wa beki wa kulia wa JKT Queens, Lidya Kabambo kujiunga na Mashujaa Queens (Amani Queens) kwa mkataba wa mwaka mmoja. Hadi sasa JKT iko tayari kumtoa beki huyo kwa mkopo kuichezea Mashujaa ambao pia ni wanajeshi wenzao kutokana na ufinyu wa kupata nafasi.