Kubweteka kisera, mawazo na mfumo wa siasa ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuviweka baadhi ya vyama tawala vya siasa katika mstari mwembamba wa ushindi au kushindwa kabisa kwenye chaguzi zilizofanyika hivi karibuni.
Kwa mujibu wa wanazuoni wa sayansi ya siasa na utawala, matokeo mabaya katika chaguzi za hivi karibuni dhidi ya vyama tawala yamechochewa na kujisahau kutimiza wajibu wao wa kuwa madarakani.
Mitazamo ya wanazuoni hao, inarejea kilichotokea katika chaguzi zilizofanyika kwenye nchi kadhaa mwaka huu, ikiwemo Afrika Kusini, Uingereza, Senegal na Ufaransa.
Katika chaguzi hizo, zilizofanyika katika miezi tofauti mwaka huu, vyama vilivyokuwa madarakani vimekumbwa na msukosuko wa ushindi, lakini vingine vimeanguka kabisa na kuvipisha vilivyokuwa vyama vya upinzani.
Chama cha ANC cha Afrika Kusini kilichoongoza kwa miaka 30, kimejikuta katika mtihani wa kushindwa kufikisha zaidi ya asilimia 50 ya kura ambazo zingekiweka madarakani bila kuhitaji kuunda serikali ya mseto.
Licha ya kuwa na mfululizo wa matokeo chanya katika chaguzi za tangu mwaka 1994, mgombea wa chama hicho cha ukombozi wa taifa hilo, Cyril Ramaphosa, katika uchaguzi wa mwaka huu ameshindwa kuendeleza historia ya chama hicho.
Katika mazingira hayo, ANC kwa mara ya kwanza kimelazimika kutengeneza Serikali ya Umoja wa Kitaifa kati yake na mpinzani wake wa muda mrefu, chama cha DA.
Hali kama hiyo imekikabili chama tawala cha Ufaransa cha National Rally (RN) ambacho pamoja na ushindi wake katika kiti cha urais, kwenye viti vya ubunge kimeanguka vibaya.
Katika uchaguzi wa duru ya pili wa nchi hiyo wa mwaka huu, muungano wa vyama vya mrengo wa kushoto vya New Popular Front (NPF), umepata viti 168 dhidi ya 143 vya RN.
Kutokana na mazingira hayo, Rais Emmanuel Macron analazimika kuunda Serikali ya Muungano, kwa maana ya kushirikiana na wanasiasa wa mrengo wa kushoto.
Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Gabriel Attal yupo mbioni kuwasilisha barua ya kujiuzulu, ingawa Macron hayupo tayari kwa hilo.
Iwapo Attal atajiuzulu, Waziri Mkuu katika taifa hilo atatokana na ushindani kutoka vyama vya siasa za mrengo wa kushoto na kulia na tayari kiongozi wa NPF, Jean-Luc Melenchon ameonyesha nia ya kukitaka cheo hicho.
Katika taifa la Senegal nako, chama tawala kimeshindwa kufua dafu dhidi ya mgombea wa upinzani, Bassirou Faye aliyepitia masaibu ya kuwekwa gerezani kwa tuhuma za kuchochea uasi, akiwa kiongozi wa upinzani.
Faye alimshinda mgombea wa chama tawala, Amadou Ba, katika uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo, akipata asilimia 54 katika kura za duru ya kwanza.
Huko Uingereza, nako chama tawala cha Conservative kimeanguka kwenye uchaguzi uliofanyika Julai, mwaka huu ambapo chama cha Labour kimerejea tena madarakani tangu kilipoongoza Serikali wakati wa Waziri Mkuu, Tony Blair (1997 – 2007).
Chama cha Labour kiliibuka na ushindi huo baada ya kupata kura 409 wakati chama cha Conservative kikipata kura 113, likiwa ni anguko kubwa kuwahi kutokea katika historia ya chama hicho.
Kufuatia kushindwa kwa chama hicho, Waziri Mkuu wa Uingereza kupitia chama cha Conservative, Rishi Sunak ameangushwa na Keir Starmer kutoka chama cha Labour amekuwa Waziri Mkuu mpya.
Kutokana na mazinmgira hayo, Mwananchi limezungumza na wanazuoni mbalimbali wa Sayansi ya Siasa, walioeleza kwa undani kilichojificha nyuma ya matokeo hayo.
Wachambuzi wa siasa wanaeleza kwamba kubweteka kwa vyama vilivyopo madarakani, kunakovifanya visiwe na mbinu mbadala au mpya za kuwashawishi wananchi ni moja ya sababu za hali hiyo, kama inavyoelezwa na mwanazuoni wa sayansi ya siasa, Profesa Ambrose Kessy.
Kwa mujibu wa Profesa Kessy, katika siasa za vyama vingi, huwa kuna ushindani na anayetawala lazima abuni mbinu mbadala.
“Inapotokea wakabweteka (chama tawala), wale washindani wanaweza wakapata ushindi,” anasema.
Hayo yote yanachochewa na kile alichoeleza, kuongezeka kwa uelewa wa wananchi, kadhalika urahisi wa upatikanaji wa taarifa za utendaji wa vyama.
“Upatikanaji wa taarifa umekuwa mwepesi na kila kinachofanyika na vyama vilivyopo madarakani vinahojiwa vikihusishwa na maana vyama, hivyo kuwa madarakani. Ikitokea vyama hivyo vimekosa majibu sahihi vinajiweka hatarini, ndicho kinachotokea,” anasema.
Profesa Kessy anasema kinachoendelea kutokea kinatoa wito kwa vyama vinavyotawala kuhakikisha vinatimiza wajibu wake, kabla havijakumbwa na adhabu kutoka kwa wananchi.
“Kwa kadri demokrasia inavyokuwa na ndivyo mbinu za wananchi kuwaadhibu watawala zinavyoongezeka. Kuna kuadhibu kupitia sanduku la kura, lakini kuna kuwaadhibu kupitia maandamano ingawa sio njia inayopendekezwa sana,” anaeleza.
Kwa mtazamo wa mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Sabatho Nyamsenda, anasema kuna mambo mawili yanayochochea misukosuko au anguko la vyama tawala madarakani.
Mwanazuoni huyo anataja sera za vyama husika kama moja ya sababu ya hali hiyo, akifafanua vingi vinatekeleza zile zinazowapa unafuu matajiri kwa maana ya sekta binafsi huku zikiwaumiza masikini.
Ukiachana na sera hizo, Dk Nyamsenda anaitaja sababu nyingine za hali hiyo ni kushindwa kwa vyama hivyo kutekeleza yale vilivyoyaahidi kwa muda wote vilipokuwa madarakani.
“Baada ya watu kupiga kura wanajikuta wanapoteza nguvu ya uamuzi juu ya nchi yao, lakini vyama hivyo havileti mabadiliko yoyote na wao wanakuwa hawana nguvu ndiyo maana wanaviadhibu kwa kutafuta vyama vyenye na sera mbadala,” anasema.
Ingawa wananchi hawana uhakika iwapo uamuzi wa kuchagua vyama vingine utawapa tija wanayoitarajia, anasema wanaamua kufanya hivyo ilimradi waone mabadiliko.
Hata hivyo, anaeleza hatari ya yanayoendelea ni kufikia wakati ambao wananchi hawataamini kama sanduku la kura linaweza kusaidia kuleta mabadiliko.
Mhadhiri mwingine wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe anasema vyama tawala vimekumbwa na changamoto ya kushindwa kusimama upande wa wananchi na kutatua kero zao hasa kupanda kwa gharama za maisha.
“Chama cha siasa lazima kiwe na utamaduni wa kubadilika kulingana na wakati hasa kusikiliza wananchi wanataka nini. Sifa kuu ya vyama vikongwe Afrika kama CCM vimeweza kusalia kuongoza dola, pamoja na sababu nyingine ambazo zinasemwa, moja kuu ni sifa yake ya kubadilika kulingana na wakati,” anasema.
Pasi na kuwa na mfumo wa kufanya mabadiliko ndani na nje ya chama kulingana na mahitaji ya wananchi, anaeleza uwezekano wa kushindwa huwa mkubwa.
“Chama pekee kitakachoweza kukaa madarakani kwa muda mrefu ni kile kinachojibu changamoto za watu wake na kutoa majibu ya kero za kila siku za watu wake,” anasema.
Mwanazuoni mwingine wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Hussein Macheta anasema vyama hivyo vinapoteza ushindi pengine kwa sababu ya kuchokwa.
Kuchokwa kwa vyama hivyo, kunasababishwa na ama vimeshindwa kutimiza matarajio ya wananchi au vimetumia ukongwe wake kama msingi wa kusalia kwake madarakani.
“Wanapaswa wawe wabunifu, waangalie wapigakura wa wakati husika ni kundi gani na wahakikishe sera zao zinaendana na kundi husika,” anasema.