Mbunge wa Mwanga (CCM) Joseph Tadayo ameanza ziara ya kukagua miradi ya maendeleo jimboni humo ikiwamo mradi wa ujenzi wa zahanati ya Kimbale iliyokuwa imekwama kwa zaidi ya miaka 20. Anaripoti Safina Sarwatt, Kilimanjaro … (endelea).
Pia mbunge huyo amekagua ujenzi wa mradi wa madarasa mawili shule ya msingi Mwero ikiwemo ofisi, choo cha matundu sita na nyumba ya walimu mbili unaondelea katika kijiji cha Mwero kata ya Kirongwe wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Mradi huo unatekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka 2024, ambapo umegharimu zaidi ya Sh 178.3 milioni.
Akizungumza katika mkutano na wananchi wa kijiji cha Kimbale baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi zahanati ya Kimbale kata ya Chomvu, amesema baada kuchaguliwa waliendeleza ujenzi wa zahanati hiyo hadi kufikia hatua ya lenta.
Amesema zahanati hiyo ikikamilika itawaondolea wananchi wa kijiji cha Kimbale adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika kijiji cha jirani.
“Wakati tumechukua uongozi huo kulikua na changamoto mbalimbali ikiwemo afya, barabara, elimu na maji na kwamba yingi zimefanyiwa kazi katika kipindi hiki cha serikali ya awamu ya sita.
“Sasa tumemaliza boma tuko kwenye lenta, hii kazi ya lenta isichukue muda mrefu… tumalize ndani ya mwezi huu wa saba,” amesema.
Amesema zahanati ya Kimbale inajengwa kwa nguvu za wananchi na fedha mfuko wa jimbo.
Akizungumza Afisa mipango halmashauri wilaya Mwanga, Hassan Wakasuvi amesema tayari wameshaliwasilisha TAMISEMI maombi ya ukamilishaji wa boma.
Miradi mwingine unaotekelezwa katika kijiji hicho ujenzi wa ofisi ya kijiji Mwero ambapo ipo katika hatua ya kupaua.
“Tunamshukuru mbunge wetu kutupatia fedha kiasi Sh milioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya kijiji cha Mwero pia tunaomba kiasi cha Sh 13 milioni ili kumalizia jengo hilo na kuanza kutumika,”walisema baadhi ya wananchi wa kijiji.
Katika hatua nyingine wananchi wa kijiji cha Mwero wameeleza Mbunge changamoto la ukosefu wa zahanati hali inayowapelekea kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Mtedaji wa kijiji cha Mwero, Cliff Mjema amesema miundombinu ya shule hiyo yalikuwa chakavu kutokana na kwamba ni jengo ya muda mrefu.
Amesema kujengwa kwa shule hiyo kutasaidia kuongeza viwango vya ufaulu kwa wanafunzi.
Mbunge huyo pia alifanya ziara katika kata ya Kig’hare na kufanya kikao cha ndani na viongozi wa chama na jumuiya zake pamoja wenyeviti wa vijiji na vitongoji.
Tadayo amesema kuna mradi mpya wa shule ya sekondari ya ufundi ambayo inatarajiwa kujengwa Kata Kug’hare na kwamba tayari serikali imeshatoa fedha.