Mil.120 za mapato ya ndani zajenga wodi 3 Mbinga

Mkurugenzi wa Idara ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Joseph Kashushura kwa kutenga fedha Shilingi Mil. 120 kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa wodi tatu ( wanaume, wanawake, watoto) zinazojengwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.

Dkt. Mfaume ametoa pongezi hizo katika ziara ya ufatiliaji na usimamizi shirikishi iliyofanywa na timu ya wataalam kutoka OR-TAMISEMI kukagua utoaji wa huduma katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Julai 9, 2024.

“Nimpongeze sana Mkurugenzi wa Halmashauri ametoa kipaumbele na kutenga fedha za mapato ya ndani sio kwamba hana vitu vingine vinavyohitaji fedha ila ameona umuhimu wa wodi hizi kwa wananchi” Amebainisha Dkt. Mfaume

Sambamba na hilo amempongeza Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kukusanya Shilingi Mil. 141 na kuvuka makisio ya makusanyo ya Shilingi Mil. 30 kwa mwaka fedha 2023/2024.

Amemtaka kufuata taratibu na miongozo ya matumizi ya fedha hizo ili kuondoa mianya ya matumizi ya fedha mbichi inayopelekea upotevu wa fedha.

Dkt. Mfaume amewataka watoa huduma wa Hospitali hiyo kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi akisisitiza kuwa huduma inayotolewa iendane na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali.

Related Posts