Mbowe aukumbuka uchaguzi wa 2015, awapa ‘kibarua’ wananchi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewataka wakazi wa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kufanya mageuzi ya kiuongozi katika chaguzi zijazo kama walivyofanya mwaka 2015.

Mbowe ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai, amesema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, chama hicho kilishinda majimbo mengi ya Kilimanjaro na Arusha, sambamba na kuongoza baadhi ya halmashauri za mikoa hiyo.

Amewataka wananchi kuonyesha mfano katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyika Oktoba mwaka huu, akiwataka wananchi hao kukinyima kura Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mwenyekiti huyo ameeleza hayo jana Jumanne Julai 9, 2024 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Himo wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro katika mwendelezo wa ziara yake ya kuimarisha chama hicho.

“Kati ya majimbo tisa ya Kilimanjaro, CCM waliambulia mawili Same Magharibi na Mwanga, lakini saba yalikwenda Chadema, hii ishara kwamba wananchi mnajitambua ingawa hamna ujasiri wa kutosha.

“Mkoa wa Arusha una majimbo saba, Chadema tulizoa majimbo sita isipokuwa moja la Ngorongoro,” amesema Mbowe.

Kiongozi huyo wa upinzani amewataka Watanzania kujifunza,  “kama ambavyo mwaka 2015 tulikaribia kuvuka, 2025 Chadema na washirika wengine wote tunaopenda mageuzi, tuna uwezo kabisa kabisa ya kuipeleka CCM likizo na kuunda Serikali nyingine.”

Hata hivyo, Mbowe amesema ili mageuzi hayo yafanikiwe lazima yatoke mikononi mwa viongozi kwenda kwa wananchi watakaokuwa sehemu za harakati za kutambua siasa ni maisha.

“Usiseme wewe sio Chadema, lakini tambua siasa ni maisha, kila mmoja ajitafakari kuwezesha mabadiliko haya,” amesema.

Katika uchaguzu mkuu wa mwaka 2015, Chadema iliyomsimamisha mgombea urais, Edward Lowassa (marehemu) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ilifanikiwa kupata majimbo 36 kutoka 23 walioyanyakua mwaka 2010.

Awali, Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini inayounda mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara, Godbless Lema amesema mfumo wa bei umesababisha hali ngumu kwa wananchi.

“Haya mambo ninayosema hayatabadilishwa na mbingu, isipokuwa binadamu anafanya uamuzi wa kubadilisha maisha, mbadala wa changamoto hizi ni chama kingine,” amesema Lema.

Related Posts