Dar es Salaam. Unaweza kusema maonyesho ya 48 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba mwaka huu ni ya kipekee kutokana na ongezeko la kampuni za kigeni zilizoshiriki zikiwamo za magari.
Maonyesho haya yanaweka upekee kwa watembeleaji pia, hasa baada ya kuwapo kwa bidhaa nyingi za kielektroniki kutoka nje kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na ofisini sambamba na nchi nyingi kushiriki.
Pia, maonyesho haya yamekuja na teknolojia mbalimbali za kilimo za ndani na nje ya nchi na viwanda vya bidhaa hasa kutoka nje ya nchi navyo vikichangamkia fursa ya kudaka soko la uhakika kwa kutangaza bidhaa zao huku wakitafuta wanunuzi wa jumla au wasambazaji wa bidhaa zao.
Mbali na hilo, wananchi wanalalamikia kutokuwapo kwa tofauti ya bei kati ya bidhaa zinazouzwa ndani ya maonyesho hayo na ile wanayonunua katika maeneo waliyoyazoea.
Ikiwa ni siku ya 11 ya maonyesho haya, mabanda yamekuwa yakishindana ubunifu katika kuhudumia wateja na namna ya kuwavutia wateja ili waweze kufika kupata huduma wanazozitoa.
Banda la Kituo cha Biashara Afrika ya Mashariki (EACLC) ni miongoni mwa yale yaliyoenda mbali zaidi katika kuvuta watembeleaji kwa kuweka skirini kubwa nje inayoonyesha shughuli wanazofanya pamoja na watu waliovalia mavazi ya roboti wakikaa nje kuvuta wateja kwa kucheza kwa staili mbalimbali.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Biashara, Exaud Kigahe, maonyesho ya mwaka huu yamekutanisha wafanyabiashara 3,846 wa bidhaa na huduma mbalimbali huku teknolojia ya hali ya juu, ubunifu na matumizi ya akili bandia (AI) yakiwa yamezingatiwa.
Kampuni za kigeni zinazoshiriki zinaonyesha teknolojia mpya za mashine mbalimbali ambazo nyingi zinahitajika kwa Watanzania katika kuanzisha viwanda vikubwa, vya kati na vidogo.
Kati ya wafanyabiashara 3,846 walioshirikia, 3,433 wanatoka ndani ya nchi huku kampuni za ndani zikiwa 3,286, wizara nane, mikoa minne, halmashauri 30, taasisi za umma 105 na 26 nchi za nje.
“Tunatarajia jumla ya kampuni za nje 413, wageni 353,201 na ajira za muda 11,712. Mwaka jana, 2023, tulikuwa na jumla ya washiriki 3,500, wakiwamo washiriki wa ndani 3,233, washiriki 267 kutoka nje, 19 kutoka nchi za nje, 10, 160 na 7ajira za muda,” anasema.
Mbali na wingi wa kampuni maonyesho hayo yamezileta nchi 26 pamoja ikiwamo Korea, Uturuki, India, Japan, Singapore, Syria, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Msumbiji, Indonesia, Mauritius, Oman, Misri, Iran, Pakistan, Rwanda, Comoro, Zambia, Ethiopia, DRC, Ghana, China, Urusi, Italia, Uganda, Kenya na Zimbabwe.
“Nawaomba wafanyabiashara wa ndani kutumia fursa hizi kujifunza teknolojia ili kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa pamoja na kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zao,” amesema Kigahe.
Alichokisema Kigahe ndiyo kilichoshuhudiwa ndani ya maonyesho hayo kwa kuwa muitiko wa kampuni za kigeni umepamba viwanja vya Sabasaba na kufanya kuonekana ya kitofauti.
Kampuni za magari na pikipiki
Kampuni za magari zilizoshiriki mwaka huu ni takribani 10 ikilinganishwa na chini ya tatu zilizokuwapo mwaka uliopita.
Ongezeko hili la kampuni za magari zilizoshiriki zilimvutia pia Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kwa kuwa alipotembelea maonyesho hayo alionyesha kuifurahia Kampuni ya Hyundai ikirejea sokoni huku akisema tangu wakati wa uongozi wake ilikuwapo.
Kwa mwaka huu pekee, chini ya Mwamvuli wa GF Trucks & Equipment’s Ltd zipo kampuni sita zilizoshiriki kwa kuuza na kuonyesha aina ya bidhaa mbalimbali za magari wanazozalisha.
Mbali na GF Automobile ambao wapo miaka yote tangu kuingia kwao nchini mwaka 2020 pia imezivuta kampuni nyingine kushiriki maonyesho haya ikiwamo Faw, Hongyan, Xcmg, Hyundai, Mahindra na Forland.
Mbali na kampuni hizo pia zipo Sinotruck, Schanman, Oho, Suzuki na Toyota.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa Kampuni ya GF Trucks & Equipment’s Ltd, Salman Karmal amesema lengo la uwepo katika maonyesho hayo ni kutaka kuonyesha kitu kinachozalishwa nchini.
Uzalishaji huo ni ishara ya uwepo wa Mazingira mazuri yanayovutia wawekezaji kuendelea kufanya kazi kwa urahisi nchini Tanzania.
Kiwanda hicho kilichoanza kazi Septemba mwaka 2020 mpaka sasa zaidi ya maroli 900 yameshatengenezwa katika kiwanda hicho kwa kutumia wafanyakazi wazawa (Watanzania) kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nje.
“Wataalamu hawa waliwafundisha vijana wetu tuliowachukua kutoka vyuo mbalimbali nchini kikiwamo Chuo cha Dar es Salaam cha Teknolojia (DIT), Chuo cha Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) na vyuo vingine vya ufundi,” amesema Karmal.
Amesema kuongezeka kwa ushawishi wa kampuni za magari kushiriki katika maonyesho haya pia kunatajwa kuwa moja ya njia inayofanya watanzania kujua bidhaa wanazoweza kuzipata nchini badala ya kuagiza kutoka nje.
Mbali na magari, pia kampuni zinazouza na kutangaza pikipiki ndogo za umeme na mafuta nazo zimeongezeka, miongoni mwake ni Sinoray.
“Mwaka huu ushindwe wewe pekee kwani pikipiki za umeme zipo za aina tofauti na watu wanashindana kwa bei, kulingana na aiba ya pikipiki unayohitaji na ukubwa wake,” amesema Nakii Daniel ambaye ni mtembeleaji wa maonyesho hayo.
Tofauti na kununua bidhaa, Sabasaba ya mwaka huu pia ni moja ya sehemu ambayo watu wenye lengo la kufanya uwekezaji huweza kupata huduma zote katika eneo moja.
Mwezeshaji Mkuu wa Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dk David Biswalo alipozungumza na Mwananchi amesema kuwapo wa kituo hicho ndani ya Sabasaba inalenga kurahisisha utoaji huduma kwa wawekezaji.
“Hizi taasisi zote zilizopo zina mamlaka ya kutoa leseni na vibali, ndiyo maana kuna hadi Wizara ya Ardhi kwa ajili ya kusaidia huduma ya kupata viwanja vinaweza kupatikana wapi, wizara ya kilimo wanaweza kuonyesha mazao ya kipaumbele yako wapi hivyo taasisi hizi zipo hapa kurahisisha kutoa huduma,” amesema.
Moja ya banda linalowezesha huduma hizo za uwekezaji, limewekwa katika banda kubwa lililokusanya kampuni nyingi kutoka China ikiwa ni moja ya hatua ya kuwawezesha wageni kufikia huduma hizo kirahisi ikiwa wataona umuhimu wa kuwekeza nchini.
Mbali na China ambayo imekuwa ikileta wafanyabiashara kutoka majimbo tofauti kwa miaka tofauti, Japan nayo inashiriki maonyesho haya ya kwanza.
Ikiwa na waonyeshaji kutoka nchini kwake, pia imekusanya baadhi ya wanufaika wa programu mbalimbali wanazozitoa nchini kwao na sasa wameanzisha biashara Tanzania.
Korea, Mozambique, nao hawajabaki nyuma mwaka huu kwani wameleta bidhaa zao mbalimbali za nyumbani, urembo, mapambo na hata kuonyesha baadhi ya shughulu wanazozifanya.
Mbali na kampuni kubwa zilizoshiriki katika maonyesho haya pia zipo zile ndogondogo ambazo baadhi zinamilikiwa na wanawake.
Wanawake hao wanaonyesha bidhaa mbalimbali zikiwamo za urembo, viungo, batiki na bidhaa za chakula.