WAKATI Ligi ya mizunguko 20 ya Caravans T20 ikihitimisha hatua ya makundi katika viwanja mbalimbali jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma, kulifanyika mechi kali ya wakali wa mchezo huo mwanzo mwa juma hili.
Mechi hiyo iliyoandaliwa na chama cha kriketi nchini(TCA), iliwakutanisha nyota ya timu ya Taifa na wachezaji wa kigeni waliong’ara kwenye ligi.
Mechi hiyo ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya kuwanoa vijana wapya wa timu ya taifa ya Tanzania na iliitwa timu ya nyota waalikwa wa TCA, ilijumuisha pia nyota wa kigeni waliokuwa wakizichezea timu zinazoshiriki ligi ya Caravans T20.
Timu hiyo ilicheza dhidi ya wazawa walioitwa hivi karibuni kuunda kikosi cha timu ya taifa ya kriketi kwenye viwanja vya Leaders Club na Waalikwa walishinda mechi zote mbili na hivyo kumpa kocha wa timu ya taifa ya wanaume, Ravish Gobind, fursa ya kupima vizuri vipaji vya wachezaji wake na kuangalia mapungufu na uwezo wa kila mchezaji.
Katika mchezo wa kwanza Waaikwa wa TCA walishinda kwa mikimbio 57 baada ya kuanza kubeti na kutengeneza mikimbio 169 huku wakipoteza wiketi 7.
Timu ya Taifa ilishindwa kufikia alama hizo baada ya wote kutolewa wakiwa wamefikisha mikimbio 112, huku wakipoteza wiketi zote 10.
Mchezaji Raunak Sharma alikuwa nyota wa mechi baada ya kutengeneza mikimbio 80 peke yake, akifuatiwa na Ajik Kayalakudi Augustin aliyeiongezea timu yake mikimbio 40.
Mchezo wa pili pia ulishuhudia Waalikwa wa TCA wakiondoka na ushindi wa mikimbio 25 na ndio waliopata kura na kuamua kufunga kwanza na kuandika mikimbio 146 huku wakipoteza wiketi tano katika mizunguko yote 20.
Juhudi za timu ya Taifa zilizalisha mikimbio 121 baada ya wachezaji wote 10 kutolewa.
Pia Kombaini ya wanawake wa TCA ilikuwa na mechi ya kukata na shoka dhidi timu ya wanaume ya Dar Tigers na Kombaini ya TCA ililala kwa wiketi 5 katika mchezo wa mizunguko 20 kwa ngazi ya daraja C.
Kombaini ya TCA ndiyo ilioanza kubeti na kutengeneza mikimbio 136 huku ikipoteza wiketi 4. Kwa ujasiri mkubwa, Dar Tigers ilizipiku alama hizo kwa kutengeneza mikimbio 137 na kupoteza wiketi 5.