Kesho katika viwanja vya Gymkhana jijini Arusha na magwiji wa gofu nchini wamenza kusaka kitita cha Sh50 milioni, kwa washindi wa raundi ya tatu ya mfululizo wa mashindano maalumu ya kumuenzi, Lina Nkya, mlezi na mwendelezaji wa gofu ya wanawake aliyefariki dunia miaka ya karibuni.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi na mratibu wa mashindano hayo yaliyopewa jina la Lina PG Tour, Yasmin Challi, yamefikia raundi ya tatu kati ya tano, lengo likiwa ni kutafuta wachezaji bora wa raundi hizo kwa ngazi ya wachezaji wa kulipwa (Mapro) na wale wa ridhaa.
“Ni michuano inayotoa kitita kinene cha pesa kwa washindi wote wa gofu ya kulipwa na ridhaa, hivyo ni wazi kutakuwepo na upinzani mkali,” alisema mkurugenzi huyo.
Alisema pia kutakuwepo na mchujo (cut) katika ngazi zote ili kupata wachezaji bora watakaocheza fainali Jumapili na zaidi ya washiriki 150 wanatarajiwa kushiriki raundi hii wakitokea mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Kilimanjaro, na Morogoro wakati wenyeji Arusha watawakilishwa na wapiga fimbo kutoka vilabu vya Arusha Gymkhana na Kili Golf.
“Kila kitu kiko sawa na Arusha inapendeza kwa uwepo wa wacheza gofu wengi,” alimaliza Challi kwa kuwakiribisha wakazi wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kuja kujionea mtifuano huu wa raundi ya tatu.
Upinzani mkali unatarajiwa kwenye raundi hiyo na mwenyeji Nuru Mollel anayeongoza kundi la Mapro atakuwa akifukuzana kwa karibu na Hassan Kadio na Fadhil Nkya, wakati kwa wacheza gofu ya ridhaa, Ally Isanzu wa TPC Kilimanjaro, aliyeshinda raundi mbili za awali, atakuwa na kibarua kigumu mbele Isiaka Daudi Mtubwi na Victor Joseph wa Dar es Salaam.
Kundi la wanawake wakiongozwa na Madina Iddi wanataka kutoa upinzani kwa wanaume katika ngazi zote za ridhaa na kulipwa.
“Nitashiriki katika kinyang’anyiro cha kusaka kitita cha pesa kwa washindi wa gofu ya ridhaa baada ya kushinda mashindano ya wazi ya wanawake nchini Zambia. Niko tayari na nimejipanga kwa hilo,” alisema Madina.
Washiriki wengine katika gofu ya ridhaa ni pamoja Vicky Elias kutoka Dar es Salaam na Neema Olomi kutoka Kilimanjaro.
Kutoka Dar es Salaam, Angel Eaton ndiye mshiriki pekee wa kike katika gofu ya kulipwa na atapambana na kina Mollel, Kadio na Nkya wanaoongoza mbio za ubingwa hadi kufikia raundi hii ya tatu.
Mshindi wa jumla wa raundi tano ataiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa yatakayofanyika Dubai mwishoni mwa mwaka.