Mke asimulia mume alivyomuaga kabla ya kujinyonga

Buchosa. Maria Ikangila, mke wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Tawi la Majengo wilayani Sengerema amesimulia mume wake alivyojitoa uhai kwa kujinyonga kutokana na ugumu wa maisha uliosababisha ashindwe kupata matibabu.

Hamis Budaga (60), mkazi wa Kijiji cha Majengo, Kata ya Nyakasungwa mkoani Mwanza anadaiwa kujinyoga kwa kutumia kamba ya nailoni kwenye mti wa mwembe ulioko nyumbani kwake.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Julai 9, 2024 saa nane usiku.

Maria akizungumzia tukio hilo leo Julai 10, 2024, ameieleza Mwananchi kuwa kifo cha mume wake kimetokana na msongo wa mawazo kutokana na uduni wa maisha wa familia yake, hivyo alishindwa kugharimia matibabu yake.

Amesema mume wake alifanyiwa upasuaji na kuondolewa nyama zilizoota puani, lakini baada ya muda hali hiyo ilijirudia hivyo alitakiwa kufanyiwa tena upasuaji akitakiwa kuwa na Sh700,000.

Amesema upasuaji huo ulitakiwa kufanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, mkoani Mwanza.

Maria amesema kukosekana fedha kwa ajili ya upasuaji huo ni chanzo cha mume wake kujinyonga kutokana na mateso ya maumivu aliyokuwa akiyapata.

“Kabla ya tukio hakulala, aliniambia mke wangu wewe lala umeteseka siku nyingi hulali, unahangaika. Mimi ninateseka na maumivu makali na wewe hulali,” amesema.

Baada ya kauli hiyo, amesema alitoka kwenda nje kama vile anayekwenda kujisaidia.

Amesema baada ya muda mrefu kupita, walitoka ndani kwenda nje kumtafuta ndipo walikuta amejitundika kwenye mti akiwa tayari amepoteza maisha.

Misungwi Hamis, mtoto wa Budaga amesema kifo cha baba yake ni pigo kwao.

Amesema hawakutarajia baba yao agejinyonga, jambo ambalo limewasikitisha.

Baadhi ya waombolezaji wakiwa nyumbani kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Tawi la Majengo, Hamis Budaga anayedaiwa kujinyonga. Picha na Daniel Makaka

Mwenyekiti wa Kijiji cha Majengo, Julius Mtwe amesema Budaga alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kuota nyama puani mara kwa mara hivyo alikata tamaa.

Baadhi ya waombolezaji wamesema iwapo angezungumza yaliyokuwa yakimkabili angeweza kupata msaada kutoka kwa jamii ya watu wanaomzunguka.

Angilina Mdilatu, mwenyekiti wa kikundi ambacho Budaga alikuwa mwanachama amesema walikuwa wanashirikiana katika za raha na shida, hivyo kifo chake kimeshtua.

Yunus Enes, ambaye ni jirani wa familia hiyo amesema kifo cha Budaga kimeleta simanzi na taharuki kwa jamii.

Ametoa wito kwa jamii licha kuwa na changamoto za kimaisha siyo vema kuchukua maamuzi ya kujinyonga, bali kuomba msaada ili watu wasaidie panapowezekana.

Diwani wa Nyakasungwa, Feruzi Kamizula (CCM) amesema kifo cha mwenyekiti huyo ni pigo kwa chama hicho katika Kata ya Nyakasungwa kutokana uchapakazi wake licha kuwa na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga amesema ana taarifa kuhusu tukio hilo, akiitaka jamii kuweka wazi mambo yanayowasibu ili kupata msaada.

Related Posts