Iringa. Hatimaye mgombea wa nafasi ya uenyekiti Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa amekabidhiwa fomu ya kuwania nafasi hiyo.
Wanawake wa Chadema Mkoa wa Iringa waliamua kwenda Jijini Mbeya kumchukulia fomu Mchungaji Msigwa wakitaka agombee nafasi hiyo anayochuana na Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amabye ni mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini.
Jana, Aprili 17, 2024 jioni, Mchungaji Msigwa amefikishiwa fomu hiyo.
Mwaka 2019, Mchungaji Msigwa alishinda uenyekiti wa kanda ya nyasa kwa kura 66 sawa na asilimia 62.5 kati ya kura 107.
Akizungumza wakati akikabidhiwa fomu hiyo Mchungaji Msigwa amesema hana nia kugombea uenyekiti wa Chadema Taifa kama inavyozungumzwa.
Amesema tetesi hizo zinazodai anataka kugombea uenyekiti Taifa huku John Heche, akitajwa nafasi ya katibu mkuu sio za kweli na zipuuzwe.
“Kumekuwa na propaganda chafu dhidi yangu moja inanihusu mimi na rafiki yangu Heche, wanasema Msigwa hana nia ya kanda anataka kugombea uenyekiti Taifa na kwamba Heche awe katibu wa chama naomba nitangaze hapa sina nia, sina mpango wa kugombea Taifa wala Heche hana mpango huo,” amesema Mchungaji Msigwa.
“Kwa sasa tunaviongozi makini kwenye ngazi ya Taifa, tunamuheshimu kiongozi wetu mkuu Freeman Mbowe makamu mwenyekiti Tundu Lissu, John Mnyika pamoja na naibu wake wa bara na Zanzibar. Tunawaheshimu tumeridhika na uongozi wao,” amesema.
Mchungaji Msigwa amesema nafasi anayogombea sio rahisi inahitaji weledi na rasilimali za kutosha ili kufanikisha utendaji kazi wa nafasi hiyo.
“Nataka niseme nashukuru Mungu kwa kuwa mwenyekiti wa kanda ya nyasa na majukumu ya kanda ya nyasa yanahitaji commitment, yanahitaji muda, yanahitaji weledi yanahitaji rasilimali na nimejitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kushirikiana na viongozi wenzangu kuyatimiza majukumu haya,” amesema Msigwa.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) Mkoa wa Iringa, Necto Kitiga amesema Msigwa hawaoni haja ya kumchagua kiongozi mwingine kwa kuwa amekuwa ni kiongozi anayefikika.
“Nawashukuru sana kwa kumthamini Msigwa ametusaidia sana katika mitizamo pia nawapongeza wanawake wa Bawacha kwa kumchukulia fomu na tunaahidi tutakuwa naye siku ya kurudisha fomu hiyo tarehe 20 kwa sababu Msigwa hatumii nguvu hatumii mabavu na anafikika kwa urahisi sana,” amesema.
Kwa upande wake, Joyce Lalika mweka hazina wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), amesema wameamua kumchukulia fomu Mchungaji Msigwa kwa kuwa anajitosheleza kwenye nafasi hiyo.
Kanda ya Nyasa inajumuisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe na Rukwa.