Masauni atangaza hadharani kuifumua Nida

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Hamad Masauni amesema halidhishwi na utendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), huku akiwaahidi wananchi kwenda kusafisha uozo ulipo.

Kauli hiyo, imetolewa baada ya kupokea kilio cha wananchi wa Ubungo jijini Dar es Salaam waliomlalamikia Waziri huyo kuwa wanamuda mrefu wanatumia namba lakini kila wakifuatilia ili wapate kadi zao wamekuwa wakizungushwa na mamlaka hiyo bila majibu.

Wametoa malalamiko hayo mkutano wa hadhara uliofanyika leo Jumatano, Julai 10, 2024, katika viwanja vya Mtaa wa Barafu, Kata ya Mburahati, Ubungo. Lengo la mkutao huo ulikuwa ni kusikiliza kero zinazowakumba wananchi kiusalama.

Waziri Masauni amesema amechoka kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kupata kadi zao huku akionyesha kukerwa na wananchi kukaa foleni kwa kuelezwa mtandao upo chini.

“Hili jambo sikutaratajia kulisikia wala litokee sasa. Ni kweli huko nyuma kulikuwa na hiyo changamoto, lakini Serikali ilitenga fedha Sh42.5 bilioni kutengeneza kadi na tulianza kuzigawa mkoa wa Mara, sasa sijajua nini kinakwamisha,” amesema.

“Inakuwaje malalamiko haya yanaendelea kujitokeza, nilikuwa Mkuranga mkoa wa Pwani juzi hali ilikuwa hiyo, nimeanzia ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo nimekuta msululu wa watu ofisi za Nida lakini nimekuja hapa malalamiko ni hayo hayo na wakati mwingine wananchi wanajibiwa mtandao uko chini,” amesema.

Waziri katika maelezo yake amesema hawezi kuvumilia watendaji wachache waendelee kuitia matope Nida, huku akiwaahidi wananchi kwenda kusafisha uozo uliopo ndani ya taasisi hiyo.

“Wote mnajua kikawaida mimi matatizo yaliyopo nchini ya taasisi zangu huwa nayamaliza kimya kimya lakini kwa hili la Nida nimechoka ngoja nilisema hapa hadharani, kwanza nakiri tunashida ila niwaahidi naenda kusafisha uozo uliopo ndani ya Nida,” amesema.

Masauni amesema katika ziara hiyo watendaji wa taasisi hiyo walipaswa kuwepo ili wajibu maswali ya wananchi lakini alishangaa kwa kutokuonekana kwao.

“Wananchi mmeona walitakiwa kuja katika mkutano huu ili wajibu maswali haya matokeo yake wamejifungia ofisini wanakula kipupwe huku wananchi wakipata shida sitaweza kulivumilia hili,” amesema.

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Nida, Geoffrey Tengeneza kutaka kujua sababu ya wao kutokuhudhuria mkutano huo, amesema: “Siwezi kujua kama viongozi wangu walikuwa na taarifa ya Waziri kuja hapo Mburahati, kwa sababu baadhi tuko huku Maonyesho ya Kimataifa ya Sabasaba.”

Awali, akitoa kilio cha vitambulisho, katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mtaa Wilaya ya Kinondoni, Razaro Mwakiposa alimuhoji Waziri huyo awaeleze inakuwaje hawapati kadi zao kwa muda mrefu sasa.

“Nida ni kero kubwa, mwananchi wanafuatilia miezi mitatu, sita hadi miaka miwili, tatizo nini Waziri kama kuna shida tunaomba utuambie na uboreshaji huduma ufanyike ili watu wapate vitambulisho haiwezekani watu tutembee na namba muda wote huu,” amesema.

Razaro ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mtaa Mkoa wa Dar es Salaam amesema katika mikutano yao na wenyeviti wenzake moja ya malalamiko ni kupata kadi huku akieleza kila wanapofuatilia hawapewi majibu sahihi.

“Umekuja katika mkutano huu na hii taasisi iko chini yako, tueleze shida nini ili tuelewe na tutoke na majibu yanayoeleweka,” amesema Mwakiposa.

Katika mkutano huo viongozi wengine waliohudhuria ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, Kamanda wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi na maofisa wengine wa Jeshi la Polisi.

Julai 4, 2024, Nida ilitangaza kuanza kuchapa upya vitambulisho vilivyochapishwa chini ya kiwango, na kuwataka wenye navyo kuviwasilisha katika ofisi zake zilizo karibu nao vichapwe upya.

Tengeneza alisema hatua hiyo imetokana na malalamiko kutoka kwa wananchi wa mikoa mbalimbali kuhusu ubora hafifu wa baadhi ya vitambulisho hivyo.

“Tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro Dar es Salaam na mingine, kuwa vitambulisho walivyopewa vimefutika picha na majina,” amesema.

Baada ya kufanya utafiti na kubaini ukweli juu ya changamoto hiyo na Nida imeamua kuvikusanya kutoka kwa wananchi ili kuvichapisha upya.

Katika mkutano huo, wananchi wamemueleza Waziri Masauni kushamiri kwa magenge ya vijana wanaovuta bangi, kupora, kukaba watu hasa majira ya usiku, na kuiba vitu vya ndani kunatokana na mfumo mbovu wa jeshi la Polisi kufanya doria na kuwaachia haraka watuhumiwa katika vituo vya Polisi.

Sango Maganga, mkazi wa Mburahati amesema mfumo wa Jeshi la Polisi kufanya doria kwa kutumia magari, kama wanatalii hawawezi kukamata wahalifu hivyo wabadilike.

“Mtaa wa barafu matukio ya watu kukabwa ni mengi, kuanzia saa mbili usiku lakini kuna magenge ya vijana wengi kuvuta bangi na wanawachora polisi wakija wanajificha wakitoka kazi inaendelea,” amesema.

Sango ameliomba jeshi hilo kubadilisha mfumo wa kufanya doria kama watalii kama wanataka kudhibiti uhalifu.

Mkazi wa Mtaa wa Kwashebe, Athuman Dede, amesema vijana katika mtaa huo wamegeuza kijiwe cha kuvuta bangi jirani na makazi yake kiasi kwamba imekuwa kero kwa familia yake.

“Wamegeuza kijiwe jirani na nyumbani kwangu moshi muda wote nina hofu huenda watoto wangu wakaathirika nimejaribu kutoa taarifa kituo cha polisi Mburahati lakini hadi sasa Waziri naeleza malalamiko kwako sijapata msaada muda wote wanakuja kuvuta,” amesema.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Ulinzi shirikishi Mtaa wa Mburahati, Daudi Mbwana amesema kufanya shughuli hiyo wanadharaurika huku wakimuomba Waziri Masauni kuwawezesha kupewa pingu na waambatane na askari katika kutekeleza majukumu yao.

Akijibu maswali hayo, Kamanda Muliro amesema kwa sasa watabadilisha mfumo wa kufanya doria badala ya kutumia magari watatembea kwa miguu ili kukabiliana na uhalifu.

“Waziri jeshi linajitahidi katika kudhibiti matukio na kukabiliana na wahalifu, mfano katika kipindi cha mwaka uliopita jumla ya watu 10 wamefungwa kifungo cha maisha na wengine miaka 30 kutoka hapa Mburahati pekee,” amesema Kamanda Muliro.

Kuhusu watuhumiwa kuachiwa haraka, Muliro amesema wao wanapenda zaidi kukaa na wahalifu lakini mifumo ya kisheria inakataa.

“Mtuhumiwa akikamatwa akafikishwa kituo cha polisi na akafikishwa mahakamani kuna kipengele cha dhamana na ni haki yake ingawa bado tunaendelea kulifanyia kazi,” amesema Jumanne Muliro.

Kwa upande wake, Waziri Masauni amesema Serikali imeendelea kujipanga katika kuimarisha ulinzi kwa kuwatengea bajeti ya Sh1.7 trilioni.

“Ni fedha nyingi na tunachokifanya ni kunoresha mazingira ya utendaji kazi wa jeshi la Polisi kwa kuwanunulia usafiri na tumeanzisha vituo vya polisi vya kata nchi nzima na tutawawezesha usafiri wa pikipiki ili watekeleze majukumu yao,” amesema.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts