WAZIRI UMMY AWASILISHA UJUMBE WA RAIS SAMIA KWA RAIS WA GUINEA

Na WAF – Guinea

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) ambae pia ni Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewasilisha ujumbe kwa Rais wa Jamhuri ya Guinea Mhe. General Mamadi Doumbouya uliotoka kwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Ummy amewasilisha ujumbe wa Rais Samia leo Julai 10, 2024 ambao umepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Guinea Mheshimiwa Dkt. Morrisanda Kouyate.

Wakati akikabidhi ujumbe huo Waziri Ummy amesema ili kudhihirisha urafiki wa kidugu kati ya Guinea na Tanzania kuna barabara kubwa katika Jiji la Dar es salaam inayoitwa Toure Road na Hospitali ya Sekou Toure iliyopo Jijini Mwanza ambao ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Tanzania wakati nchini Guinea kuna Chuo Kikuu cha Julius Nyerere University of Kankan (UJNK).

“Naishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Guinea kwa mapokezi mazuri ambayo yamedhihirisha ushirikiano wetu wa karibu na hatimaye kupokea ujumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.” Ametoa shukrani hizo Waziri Ummy

Wakati akipokea ujumbe huo kutoka Nchini Tanzania kwa niaba ya Rais wa Guinea, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Guinea Mheshimiwa Dkt. Morrisanda Kouyate amesisistiza kuwa, Jamhuri ya Guinea itaendelea kutambua ushirikano wa kidugu na wa muda mrefu kati ya Guinea na Tanzania ulioanzishwa wakati wa waasisi ya Mataifa hayo Mawili, Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere na Mhe. Ahmed Sekou Toure.

Related Posts