Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema licha ya usajili wa mastaa waliosajiliwa katika timu hiyo, hana hofu ya kupanga kikosi.
Gamondi amesema kikosi kitakuwa kinapangwa kulingana na aina ya wapinzani wanaokutana nao.
Amesema mbali na wapinzani, pia itategemea na viwango vya wachezaji ili kutumika kwenye michezo husika.
“Ugumu wa kupanga timu? Hapana. Hakuna ugumu, timu inapangika sioni wasiwasi kabisa, inategemea na mpinzani utakayekutana naye,” amesema Gamondi.
“Mimi sio mtu ninayepanga timu kwa kuangalia majina ya wachezaji, inategemea kiwango cha mchezaji. Kuna wakati utahitaji kucheza na viungo wawili wakabaji, wakati mwingine washambuliaji wawili, wakati mwingine viungo washambuliaji wawili au watatu.
“Kuna wakati unaweza kumpa nafasi Azizi (Stephanie) acheze, ukampumzisha mwingine au wakati mwingine ukawatumia wote, ligi ni ndefu na mechi ni nyingi.”
Yanga ilimaliza Ligi Kuu Bara msimu uliopita ikiwa bingwa wa mashindano hayo na Kombe la Shirikisho (FA).