Kilosa. Watu watatu wakiwemo raia wawili wa Burundi wamefariki dunia baada ya lori kugongana na gari ndogo na kisha kuwaka moto.
Lori hilo lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Burundi liligongana na Toyota Harrier, kisha kuwaka moto usiku wa kuamkia Julai 9, 2024 eneo la Kwambe barabara kuu ya Morogoro -Dodoma.
Miili miwili imepatikana baada ya kichwa cha lori kunyanyuliwa kikiwa kimeungua.
Waliofariki dunia wametambuliwa kuwa ni Izombingomba Leonard (67), dereva wa lori, na msaidizi wake Ntorenganya Modeste (37), wote raia wa Burundi.
Miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Dumila wilayani Kilosa.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Julai 10, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amesema dereva wa Toyota Harrier, alifariki dunia akipatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo na jina lake bado halijatambuliwa.
Amesema ajali hiyo ilitokea Julai 9, saa moja kasoro usiku baada ya dereva wa gari dogo katika kukwepa ajali aligonga mti na baadaye kugonga lori lililokuwa limebeba vigae.
Shaka amesema baada ya kugongwa lori lilipinduka na kuwaka moto.
Shaka amewashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kazi kubwa waliyofanya ya kushiriki kutoa miili hiyo na kuwa waaminifu kwa kulinda mali iliyokuwa imebebwa kwenye lori hilo.
Dickson Sekwao, mkazi wa Kwambe aliyeshuhudia ajali hiyo, amesema siyo ya kwanza katika eneo hilo, hivyo ameiomba Serikali kuweka vidhibiti mwendo.
John Sylvester, mkazi wa eneo hilo ameiomba Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka matuta eneo hilo lenye kona kali.
Amesema ajali zimekuwa zikitokea kutokana na mwendo kasi wa madereva pasipo kuchukua tahadhari.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shaban Marugujo amesema taarifa kuhusu ajali zilichelewa kufika ofisini kwao lakini walifika eneo la tukio na kuzima moto.
“Ni kweli tulipata taarifa za uwepo wa ajali hiyo iliyosababisha moto kwenye lori, tulipofika eneo la tukio tulikuta moto umeshateketeza sehemu kubwa ya lori,” amesema.