Chuku: Huyu Bocco bado sana!

SIMBA imeachana na aliyekuwa nahodha wa timu hiyo ambaye amehudumu kwa miaka sita ndani ya kikosi hicho akitwaa mataji ya ndani wakiaamini atastaafu, lakini mambo yamebadilika kwani ameibukia JKT Tanzania.

Wakati staa huyo mwenye rekodi nzuri kwenye eneo analocheza bado hajaanza kibarua cha kuitumikia timu yake mpya ya JKT Tanzania, aliyekuwa beki wa Pamba, Salum Abdallah ‘Chuku’ amemkingia kifua kwa kuweka wazi bado ana muda wa kucheza.

“Inashtua kuzungumzwa Bocco umri umeenda, nawahakikishia ataenda kufunga sana JKT Tanzania kwani kwa nafasi yake hakuna mchezaji ambaye anamuweza, ni mshambuliaji ambaye ana jicho la kuona goli,” anasema Chuku ambaye alifunguka mambo mbalimbali ikiwamo kumpa maua yake nahodha wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Beki huyu ambaye amemaliza mkataba na Pamba sasa ni mchezaji huru na anamtabiria makubwa mshambuliaji huyo ambaye alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana ya Simba na anatajwa kutua JKT Tanzania;

 “Wanaona Bocco ni mtu mzima jamani, hivi wanamfahamu mshambuliaji wa klabu ya Red Arrows FC ya Zambia, James Chamanga mwenye umri wa miaka 50 sasa kama sijakosea na bado anafunga,” anasema na kuongeza;

“Ushambuliaji sio kazi kubwa kwani ni kutambua tu namna ya kujitenga ndani ya boksi kitu ambacho kinafanywa sana na Bocco na bado hana umri wa kumfanya akaombwa kustaafishwa, kwa sasa bado tunamhitaji kwenye Ligi Kuu Bara,” anasema Chuku.

Chuku anasema Bocco bado ana miaka mingi ya kucheza huku akithibitisha kama Chamanga anatupia na kuwaacha washambuliaji wenye damu changa, haoni kama hilo litamshinda nahodha huyo wa zamani wa Simba.

Chuku anasema miongoni mwa mabeki bora wa kushoto Ligi Kuu Bara ambao wamemudu kucheza misimu zaidi ya mitano kwa kiwango ni pamoja na beki wa kushoto wa Simba, Mohammed Husein ‘Tshabalala’.

Beki huyo amemmwagia sifa zake ni miongoni mwa mabeki bora na mwenye nidhamu ya mpira.

Tshabalala amehudumu Simba kwa misimu 14 sasa akitwaa mataji yote ya ndani na amecheza eneo lake kwa ubora akiitumikia Simba na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’na Chuku anasema ni mchezaji anayetakiwa kupewa maua yake.

“Nafasi anayocheza ni ya kutumia nguvu na maarifa hilo wala halimpi shida, amekuwa akipambana kuisaidia timu kupandisha mashambulizi na baadae kurudi nyuma kukaba lakini bado unamwona kila msimu anakuwa bora,” anasema na kuongeza;

“Sio rahisi kufanya kazi kama anayofanya Tshabalala na ukaendelea kuwa bora zaidi ya misimu minne hadi mitano mfululizo tofauti na wachezaji wa timu nyingine, anastahili kupewa maua yake na wachezaji wanaochipukia wamtazame na kujifunza vitu,” anasema Chuku.

MASHABIKI WANAUA WASHAMBULIAJI

Chuku anasema washambuliaji wazawa wamekuwa wakiibuka na kupotea kila mara na hii ni kutokana na hofu kwa mastraika wakihofia mashabiki ambao wanakuwa sio wavumilivu.

“Washambuliaji wapo wengi na wamekuwa wakifunga sana mazoezini lakini kwa asilimia kubwa wameamua kukimbia nafasi zao na kuchagua maeneo ambayo sio sahihi kutokana na hofu ya mashabiki wa Tanzania ambao hawana uvumilivu,” anasema na kuongeza;

“Mshambuliaji anapata nafasi ya kucheza akikosea tu anazomewa hii tabia ndio inakimbiza mastaa wengi ambao wangeweza kulipambania Taifa kwani wanaamua kukimbia nafasi hiyo na kujificha kwenye kivuli cha mawinga na viungo washambuliaji,” anasema.

Chuku anasema mazoezini wamekuwa wakifanya mazoezi ya kufunga na kufanya vizuri lakini linapokuja suala la kupangwa eneo la ushambuliaji wanakataa na kujipa nafasi ambazo wanaamini hazitakuwa na maneno mengi kutoka kwa mashabiki na kuwafanya wakatoka mchezoni.

Amecheza msimu mmoja tu Ligi ya Championship lakini Chuku ameapa hawezi kurudi huko tena hata wamtengee fedha nyingi kiasi gani.

“Msimu mmoja wa Championship ni sawa na misimu miwili ya Ligi Kuu Bara hii ni kutokana na nguvu kubwa inayotumika kwenye mechi za madaraja ya chini hasa timu iliyo na mipango ya kupanda ligi kama ilivyokuwa kwa Pamba,” anasema na kuongeza;

“Kucheza Championship unatakiwa kuwa kwenye hali ya utimamu zaidi ligi ya kule ni ngumu tofauti na Ligi Kuu Bara ambayo hata mkipoteza mchezo mmoja mnajua mtajipanga kusawazisha makosa mechi inayofuata lakini kule kila mchezo ni fainali hasa kama timu yenu ina malengo ya kupanda,” anasema na kuongeza timu iliyokuwa na mipango ya kupanda wachezaji hawachezi kwa ajili ya kuonyesha uwezo zaidi wanapambania matokeo na wanakuwa na ligi binafsi.

Wakati timu zikisafiri kwenda mikoa au nchi nyingine kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya, wadau na mashabiki wakifurahia, basi unaambiwa wachezaji cha moto wanakiona na wala hawafurahii kama anavyothibitisha Chuku.

“Hakuna kazi ngumu au mazoezi magumu kama ya mwanzo wa msimu ‘Pre Seasson’ huu ni mtiani ambao tunaukimbia wachezaji wengi kutokana na ugumu tunaokutana nao huko, kuna mazoezi magumu sana ambayo sio wachezaji wengi wanamudu kuyafanya na ni lazima kila mmoja afanye,” anasema na kuongeza;

“Muda huu wa mapumziko ndio maana wachezaji wengi wanatamani kutoka na kwenda nje na miji yao ili wakapate muda wa kupumzisha miili yao baada ya kazi ngumu ya kucheza mechi za msimu mzima lakini ukweli wanatambua mwezi mmoja na wiki kadhaa walizozipata watarudi kuzitumikia kwa ugumu kwenye maandalizi ya msimu mpya.”

Chuku anasema kuna utofauti mkubwa kati ya kujiandaa na mechi na kujiandaa na msimu mpya mazoezi yake ni magumu na ni tofauti akiweka wazi kujiandaa na mechi wanaweza kufanya kwa kuzingatia mpinzani wanayekwenda kukutana naye lakini kujiandaa na msimu wanafanya kila kitu.

KILIMO, UFUGAJI HUMKAMATI

Kila mwanadamu ana malengo yake wakati wengine wamewekeza nguvu kwenye soka, kwa upande wa beki Chuku amethibitisha soka anacheza kwa sababu ya kipaji na mapenzi nao lakini nguvu zake nyingi kawekeza kwenye kilimo na ufugaji.

“Mimi ni mzaliwa wa Geita lakini sijawahi kuwekeza nguvu kwenye uchimbaji madini kwa sababu ni kazi inatumia muda mwingi, mimi nimeamua kulima na kufuga,” anasema na kuongeza;

“Nina hekari 20 za shamba, nalima mpunga na nafuga kuku wa nyama ambao ninao zaidi ya 3000, nimekuwa nikifanya biashara hiyo nje na soka na imenibadilishia maisha yangu japo soka pia limekuwa likinisogeza,” anasema.

Related Posts