KLABU ya Singida Black Stars, iko katika mazungumzo ya mwisho ya kupata saini ya beki wa kulia wa Asec Mimosas, Ande Cirille Habib.
Nyota huyo inaelezwa tayari yupo nchini ili kukamilisha uhamisho wake na endapo dili lake litakamilika, basi atakuwa ni mchezaji wa tatu kujiunga na miamba hiyo baada ya beki wa kati, Anthony Tra bi Tra na kiungo, Josaphat Arthur Bada.
Kikosi hicho kwa sasa kinashiriki michuano ya Kombe la Kagame inayoendelea kupigwa jijini Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya msimu ‘Pre Season’ kikiwa chini ya Kocha Mkuu Mbelgiji, Patrick Aussems aliyewahi kufundisha timu mbalimbali ikiwemo Simba.
UONGOZI wa Azam FC uko katika mazungumzo ya kupata saini ya beki wa kulia wa FC Les Aigles du Congo, Dieumerci Mukoko Amale.
Beki huyo aliyewahi kukichezea kikosi cha Difaa El Jadida cha Morocco, inaelezwa tayari makubaliano binafsi yamefikiwa kwa kiasi kikubwa na kilichobaki kwa sasa ni mambo madogo tu ya kukamilisha uhamisho wake ili aweze kutua hapa nchini.
TIMU ya Kagera Sugar, iko katika mazungumzo ya kupata saini ya kiungo mkabaji, Athuman Maulid Rajab ambaye yupo huru.
Maulid kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini chini ya miaka 23 na msimu uliopita alikuwa akiichezea timu ya Volcano ya Comoro, huku akipita pia Mwadui FC na Fountain Gates.
MABOSI wa Al Hilal ya Sudan wameanza mazungumzo ya kunasa saini ya kiungo wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’, Greyson Gwalala.
Nyota huyo amekuwa akiwavutia mabosi wa matajiri hao ambao mara ya kwanza walimtaka katika dirisha dogo la Januari, mwaka huu ila walishindwa kufanikiwa na sasa inaelezwa wamerudi tena.