BARCELONA, HISPANIA: LAMINE Yamal. Ndiyo jina linaloitikisa kwa sasa duniani. Hakuna asiyemjua kijana huyu wa umri wa miaka 16 tu. Anayoyafanya huko kwenye michuano ya Euro, Ujerumani ni balaa.
Kwenye mchezo wa juzi Jumanne wa Hispania dhidi ya Ufaransa alifunga bao moja kati ya mawili kwenye ushindi wa mabao 2-1 na kuweka rekodi ya kuwa kijana mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao kwenye historia ya michuano hiyo (miaka 16 na siku 362).
Angeingia kwenye historia nyingine ya kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kucheza mchezo wa fainali lakini kwenye mchezo huo ambao Hispania imefuzu na ilikuwa inasubiri mshindi wa jana kati ya Uholanzi dhidi ya England, atacheza akiwa ameshafikisha umri wa miaka 17.
Kwa rekodi hiyo, ameipita ya staa wa zamani wa Uswisi, Johan Vonlanthen aliyefunga bao akiwa na umri wa miaka 18 na siku 141.
Kwenye michuano hiyo hadi sasa kinda huyo wa Barcelona amecheza jumla ya mechi sita akifunga bao moja na kutoa asisti tatu.
Kwenye mchezo huo wa juzi, alicheza jumla ya dakika 89, akitoa pasi sahihi 23 na kupiga mashuti matatu, moja likizama wavuni.
Kabla ya michuano hiyo, msimu uliopita alionyesha kiwango bora akiwa na Barcelona akifunga mabao saba na kutoa asisti 10 katika mechi 50 za michuano yote.
Lamine alijiunga na Barcelona akiwa na umri wa miaka saba na kukuzwa katika kituo cha michezo cha klabu hiyo cha La Masia kabla ya kupandishwa rasmi Aprili mwaka jana na alicheza mechi yake ya kwanza na wababe hao akiwa na umri wa miaka 15 na siku 290, akiwa ndio mchezaji mdogo zaidi kuwahi kuchezea timu hiyo baada ya karne moja kupita.
Mashabiki wa Barca na viongozi wengi wa timu hii wanamwona ni Lionel Messi mpya kwenye kikosi chao, ikichagizwa na picha inayosambaa mitandaoni hivi karibuni ikimwonyesha staa huyu akiogeshwa na Messi katika picha za kutengeneza kalenda ya mwaka ya Barcelona. Wakati huo Lamine alikuwa na miezi minne.
Kutokana na kiwango chake timu nyingi zinataka saini yake na hilo limeifanya liweke katika mkataba wake kipengele kinachoitaka timu inayomtaka itoe Pauni 868 milioni kama ada ya uhamisho.
Kabla ya kuamua kuichezea Hispania, staa huyu aliyezaliwa mwaka 2007, alikuwa na chaguo la kuichezea Morocco ambako baba yake ametokea ama Equatorial Guinea anakotokea mama yake.
Mara kadhaa Morocco imekuwa ikimshawishi baba yake amruhusu staa huyu kuchezea taifa lao, kabla ya Hispania kumuwahi na kuzichezea timu za taifa za timu hiyo za umri tofauti kabla ya kuichezea ya wakubwa akiwa na umri wa miaka 16 na siku 57 pekee akiweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kulitumikia taifa hilo.
Kwa sasa anapokea mshahara wa Euro 32115 kwa wiki na kabla ya huo alikuwa akilipwa Euro 70 kwa wiki.
Mbali ya soka Lamine bado anasoma na akiwa kambini katika michuano hii alikuwa akijisomea mwenyewe na kufanya baadhi ya mitihani aliyopewa.
Ilitangazwa staa huyo amefaulu mtihani wa ESO sawa na kidato cha sita kwa hapa Tanzania.
Kwa muda mwingi amekuwa akipokea sapoti kubwa kutoka kwa familia yake hususan baba yake ambaye mara zote huwa naye bega kwa bega popote kule anakoenda kucheza mechi, tangu akiwa mdogo hadi sasa.