Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema ni muhimu kufanya utafiti wa kisayansi kusaidia kukwamua changamoto za uzalishaji sekta mbalimbali ikiwemo elimu na kilimo, kwa lengo la kuchochea ustawi endelevu wa maendeleo kiuchumi.
Amesema hayo jana Julai 10, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika ufunguzi wa mkutano mkuu, unaojadili ushahidi wa matokeo ya utafiti.
Ili kufikia azma hiyo amewahimiza watafiti kufanya tathmini muhimu kwa kuzingatia mambo makuu matatu, ikiwamo kuangalia mwenendo wa idadi ya watu katika nchi, ili kuwa na mipango mizuri na yenye manufaa kwa Taifa.
‘’Tafiti zinapaswa kusaidia kutatua changamoto zinazokabili makundi mbalimbali ikiwemo wazee na vijana kwa kuzingatia kipaumbele vyao,” amesema.
Jambo lingine amewataka wataalamu wa uchumi na wadau wa maendeleo, kuisaidia jamii kutumia teknolojia kwa manufaa chanya pamoja na kukabiliana na mabadiliko hayo.
Pia amewasisitiza kufanyia tathmini ya mara kwa mara sera zinazotungwa na kutekeleza, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa ya muda mrefu.
Mkutano huo umeandaliwa na Taasisi ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ESRF) na kushirikisha mashirika mbalimbali ya kimataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Profesa Fortunata Makene, amesema mkutano huo umewakutanisha watafiti kutoka sehemu mbalimbali duniani, ukilenga kupokea mawasilisho ya utafiti na kuangalia namna matokeo ya tafiti hizo yanavyoweza kutumika kusaidia watunga sera.
Amesema mkutano huo ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za kitafiti za kimataifa na Afrika, kwa kuwezesha upatatikanaji wa taarifa mahususi ili kusaidia mipango ya nchi.