MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) inaendelea jijini Dar es Salaam. Hii ni moja ya michuano ya muda mrefu ya klabu Afrika.
Awali yalijulikana kama Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati na baadae mwaka 2002, yaliitwa Kombe la Kagame baada ya kudhaminiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye ni shabiki mkubwa wa soka.
Miaka ya nyuma mashindano haya yalikuwa ni kalenda muhimu sana kwenye soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Uhuru wa Afrika Kusini mwaka 1994 na kabla ya hapo kuundwa kwa Shirikisho la Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa) mwaka 1983 kulipunguza kwa kiasi kikubwa nguvu kwani klabu kutoka ukanda huo kama Zambia, Malawi na Zimbabwe zikajiondoa kwenye michuano hiyo.
Klabu kama Limbe Leaf, Admarc Tigers za Malawi, Mufulira Wanderers ya Zambia, Rio Tinto na nyinginezo zilileta chachu katika mashindano haya.
Klabu za Tanzania, Kenya na Uganda zimekuwa zikipokezana ubingwa wa michuano hiyo mara nyingi. Simba na AFC Leopards zimebeba mara 6, Yanga na Tusker Kenya Mara 5 sawa na Gor Mahia, huku Al Merrikh (Sudan) na Sports Club Villa zimechukua mara 3 kila moja.
Kwa hapa Tanzania Simba, Yanga na Azam zimechukua kombe hilo kwa pamoja mara 13, huku timu za Kenya zikigawana mara 16.
Kwa mara ya kwanza michuano hiyo inafanyika katika ardhi ya Tanzania bila kuzishirikisha klabu za Yanga, Simba na Azam FC.
Hii inaweza kuwa ni mara ya kwanza michuano kufanyika ndani ya Tanzania bila msisimko uliozoeleka tangu miaka ya 1970.
Michuano ya Kagame kama ilivyo kwa Kombe la Chalenji inayohusisha timu za taifa imekuwa ni kama homa za vipindi.
Anapotokea mfadhili au mdhamini wa kutia msukumo michuano inapofanyika, nguvu hiyo ikipungua basi mwaka huo hakuna kuchezwa na kikwazo kikubwa ni fedha.
Pia kalenda ya michuano hiyo ni tatizo. Miaka ya nyuma michuano hii ilifanyika mwanzoni mwa Januari kwani msimu wa ligi nyingi hapa Afrika zilianza mwanzoni mwa mwaka na klabu zilitumia michuano hiyo kujiandaa na ligi za nyumbani na za kimataifa.
Baada ya kalenda ya kimataifa kwa mashirikisho mengi kuanzia katikati ya mwaka, ikabidi mashindano yafanyike kwenye nusu ya pili ya kalenda ya mwaka yaani kuanzia Julai.
Ukiangalia kwa timu iliyomaliza msimu wake Juni na kutakiwa kucheza mashindano ya kimataifa Julai ni mtihani kweli kweli.
Wachezaji ni binadamu na wanahitaji mapumziko baada ya msimu mrefu wa ligi. Pia, msimu unapoanza wachezaji wanakuwa hawajarudi katika utimamu wa mwili, jambo ambalo ni hatari kwa afya kama wataingizwa viwanjani.
Mashindano kufanyika Julai wakati klabu zinafanya kambi kujiandaa na msimu, bado si afya sana. Labda Agosti ungekuwa mwafaka kwani wachezaji wanakuwa wamepata utimamu na klabu pia zinakuwa na mahitaji ya michezo ya kuzijenga timu zao. Sijui ni kwa nini Cecafa kwa mfano walipopanga mashindano ya mwaka huu jijini Dar Es Salaam hawakulizingatia hilo.
Changamoto nyingine inayoyakabili mashindano haya ni kukosa ufadhili na udhamini wa kutosheleza na kushawishi klabu kushiriki mashindano haya.
Zamani klabu ziliona fedha iliyokuwa inapatikana kwenye mashindano haya, baada ya kuingia Rais Kagame ni kubwa. Kwa sasa fedha ya Mzee Kagame, bila kukosea heshima hisani hiyo, hatuwezi kusema inashawishi klabu kushiriki mashindano hayo.
Dola 30,000 anazopata bingwa wa Kagame Cup yawezekana haifikii hata fedha anayopata mshindi wa tano wa NBC Premier League. Inashangaza tangu mwaka 2002 bado Cecafa inategemea Dola 60,000 za Mzee Kagame kama mwokozi pekee kwa fedha za zawadi za washindi.
Dola 30,000 inayotolewa leo bado ni sawa na kiasi cha Dola 30,000 ilizopokea Yanga mwaka 2011 na mwaka 2012 kwa kushinda kombe hilo? Angalia ni kiasi gani timu hupokea kwa kuingia hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa ya CAF au hata kombe la shirikisho? Hakika Dola 30,000 haziwezi kushawishi timu zenye matumaini ya Afrika kusafiri kuyafuata mashindano.
Ninavyoandika hivi, wenyeji Yanga na Azam wamekwishatangaza kutokuwemo kwenye mashindano haya. Ninavyoandika hivi Simba wako kambini Misri wakijifua kwa ajili ya msimu mpya wa ligi. Ninapoandika hivi klabu ziko bize zikikamilisha usajili.
Matokeo ya haya yote ni nchi nyingi zinaweza zisiwakilishwe na zikiwakilishwa zitaleta vikosi dhaifu au timu ambazo hazikuwa chaguo la kwanza. Ikumbukwe hii ni ligi ya mabingwa ya Afrika ya Mashariki na Kati. Ni mabingwa wangapi watashiriki? Hapa kuna hatari ya mashindano haya kususiwa na walioitwa na kuitikiwa na wasioitwa. Inakuwa hadithi ya biblia ya bwana aliyealika watu wengi kisha kila mmoja akatoa kisingizio chake cha kutokuwepo kama nimeoa, nimenunua maksai, nimenunua shamba na mengine.
Nasikia Cecafa ina sekretarieti pale Nairobi ambayo iko chini ya Katibu Mkuu. Sijui mambo yamebadilika kiasi gani kutoka enzi ya Nicolas Musonye ambaye kusema ukweli alikuwa ndiye Cecafa na Cecafa ilikuwa yeye. Aliendesha ofisi kama shamba binafsi. Musonye alifanya maamuzi bila hata ya kuhitaji vikao. Haya yote yalitokana na ukweli kilichoitwa sekretarieti ya Cecafa kilikuwa na labda bado kipo kwenye maandishi tu. Ikiwa ukweli bado ni kama ninavyojua, itachukua muda mrefu kwa klabu kubwa kwenye ukanda huu kuvutika kushiriki Cecafa Kagame Cup. Cecafa inatakiwa kujifunza jambo moja au mawili kutoka kwa wadogo zao wa Kusini mwa Afrika yaani Cosafa ili kusonga mbele kwa namna ya kuendesha ofisi ya shirikisho, namna ya kuendesha na kuboresha mashindano na kuleta maendeleo ya soka katika ukanda wao kwa jumla.
Mwandishi wa makala haya ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).