AKILI ZA KIJIWENI: Andabwile, Kagoma nisikilizeni kwa umakini

DIRISHA la usajili lilichangamka sana wiki hii hasa kwa timu mbili vigogo nchini Simba na Yanga ambazo zilitambulisha baadhi ya wachezaji wao na wengine zikawapa ‘Thank You’.

Miongoni mwa wachezaji waliotambulishwa ni viungo wawili wakabaji, Yusuf Kagoma na Aziz Andabwile ambao msimu uliopita walikuwa wakiitumikia Singida Fountain Gate.

Aziz Andabwile alitambulishwa na Yanga ikionekana ni usajili uliofanywa kwa ajili ya kuziba pengo la Zawadi Mauya aliyeachana na timu hiyo na kujiunga na Singida Black Stars.

Rafiki yake ambaye walikuwa wanacheza pamoja, Yusuf Kagoma alitambulishwa na Simba akionekana kama usajili wa kuchukua mikoba ya Hamis Abdallah ambaye klabu hiyo itaachana naye katika dirisha hili.

Hawa ni wachezaji wazuri sana kutokana na kiwango walichokionyesha katika timu walizozichezea hapo nyuma kabla ya kujiunga na Yanga na Simba.

Hata hivyo, nawakumbusha Andabwile na Kagoma wasiishi kimazoea katika timu walizoenda na kudhani tayari wameshayapatia maisha ya kisoka na kuanza kubweteka kama ambavyo wenzao wengi wamewahi kufanya hapo nyuma.

Simba na Yanga ni timu zenye presha kubwa ya matokeo mazuri na muda wote zinahitaji mchezaji awe katika kiwango bora ili atoe mchango chanya na kinyume na hapo hazisiti kumuonyesha mtu mlango wa kutokea zinapoona hana msaada.

Wajitahidi kufanya mazoezi na kila wanapopata nafasi katika mechi waonyeshe viwango vizuri vitakavyowashawishi makocha wao kuwapa nafasi ya kucheza mara kwa mara jambo litakalolinda nafasi zao klabuni kwa muda mrefu.

Wakiwa wachezaji muhimu watavuna mamilioni ya fedha ndani ya timu hizo na watakuwa vipenzi vya mashabiki na wapenzi wa Yanga na Simba ila kinyume na hapo mambo yatakuwa magumu kwao.

Related Posts