Kilosa. Ndugu wa raia wawili wa Burundi waliofariki dunia kwenye ajali ya lori iliyotokea juzi katika eneo la Kwambe, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wamefika Kilosa na kutambua miili hiyo.
Marehemu hao ni Izombingomba Leonard (67), aliyekuwa dereva wa lori na Ntorenganya Modeste (37), aliyekuwa dereva msaidizi ambao walifariki dunia baada ya lori walilokuwemo kugongana na gari dogo aina ya Toyota Harrier kisha kupinduka na kuwaka moto.
Lori hilo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Burundi, likiwa limebeba shehena ya vigae.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 11, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema ndugu wa marehemu hao wamefika Kilosa usiku wa jana na tayari wameitambua miili ya wapendwa wao.
“Baada ya kuitambua miili hiyo, kwa sasa ndugu hao wanaendelea na taratibu za kuisafirisha kwenda kwao kwa kuzika, sisi kama Serikali tunaendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha ili wawasafirishe ndugu zao,” amesema Shaka.
Kuhusu aliyekuwa dereva wa gari dogo, Shaka amesema naye tayari mwili wake umetambuliwa na ndugu zake na sasa wanaendelea na taratibu za kusafirisha mwili huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amewataka madereva wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari hasa katika maeneo ambayo yanaonekana hatarishi, yakiwemo yenye kona na miteremko mikali ili kuepuka ajali zinazopoteza maisha ya watu na uharibifu wa na vyombo vyenyewe vya usafiri.