TIMU za kikapu ya Srelio na Crows zimeanza kuzitisha timu zinazoshiriki ligi ya kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BDL), baada ya kushinda katika mchezo wao wa kwanza wa mzunguko wa pili wa ligi hiyo uliopigwa kwenye Uwanja wa Don Bosco Youth Centre.
Vitisho vya timu hizo vimetokana na timu ya Srelio kuifunga timu ya Vijana ‘City Bulls’ kwa pointi 78-64, huku Crows nayo ikiifunga Chui kwa pointi 76-69
Katika mzunguko kwanza timu ya Srelio ilimaliza mzunguko wa kwanza, katika nafasi ya 14 na Crows ikiwa ya 16 ya mwisho.
Timu ya Srelio ilianza mchezo taratibu katika robo ya kwanza huku ikiisoma timu ya City Bulls.
Hadi robo iyo inamalizika City Bulls ilikuwa inaongoza kwa pointi 16-13, robo ya pili Srelio nayo ikaongoza kwa pointi 24-17, 20-15,21-16.
Katika mchezo huo Sponican Ngoma alifunga pointi 21 na kati ya pointi hizo alifunga katika maeneo ya mitupo ya pointi tatu (three pointer) mara 5 na pasi mbovu alitoa mara mbili (turnover).
Aliyemfuatia alikuwa Chaly aliyefunga pointi 14, huku Fotius Ngaiza kutoka timu ya ‘City Bulls’ akifunga pointi 17.
Miyasi Nyamoko nahodha wa timu ya Srelio, alisema ushindi huo kwa upande wao ulikuwa ni muhimu kwao kutokana na nafasi waliyokuwa nayo katika mzunguko wa kwanza.
Kwa upande wa kocha wa timu ya Crows, Abasi Sanawa alisema ushindi wao ulichangiwa na mazoezi waliyokuwa wanafanya.
Mchezo mwingine uliochezwa kwenye Uwanja wa DB Oysterbay, ABC iliifunga DB Oratory kwa pointi 68-58.